Wanawake Waislamu nchini Myanmar wananajisiwa na askari
Makumi ya wanawake Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wanasema wanajeshi wa serikali wamekuwa wakiwanajisi na kuwadhalilisha kijinsia.
Tayari wanawake wanane kutoka kijiji cha U Shey Kya katika jimbo la Rakhine wamesimulia namna ambavyo wiki jana askari waliwanajisi wakiwa wamewaelekezea bunduki huku wakihujumu nyumba zao na kuzipora.
Utawala wa Myanmar uliwatuma wanajeshi katika jimbo la Rakhine mapema mwezi huu baada ya madai kuwa wakaazi Waislamu wa eneo hilo wamewashambulia polisi.
Mwanamke wa miaka 40 amesimulia namna wanajeshi wanne walivyomnajisi na kumpiga bintiye wa miaka 15 huku wakipora dhahabu na fedha alizokuwa nazo.
Wanaume wametoroka kijiji hicho kwa kuhofia kukamatwa kwa madai kuwa ni wanamgambo. Wanawake waliobaki kijijini kulinda nyumba na mali sasa wananajisiwa na wanajeshi.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa Waislamu wa kabila la Rohingya ni jamii ya wachache duniani inayodhulumiwa na kunyongeshwa zaidi. Serikali ya Myanmar inakataa kuwapa haki za uraia Waislamu ambao idadi yao ni zaidi ya watu milioni moja na laki tatu.
Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Thailand, Malaysia na Indonesia kutokana na mashambulio ya Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.