Waislamu Warohingya 150 wauliwa katika shambulio la jeshi la Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i19636-waislamu_warohingya_150_wauliwa_katika_shambulio_la_jeshi_la_myanmar
Waislamu wasiopungua 150 wa jamii ya Rohingya wameuliwa katika mashambulio yaliyofanywa na jeshi la Myanmar katika eneo la Rakhine.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 17, 2016 07:24 UTC
  • Waislamu Warohingya 150 wauliwa katika shambulio la jeshi la Myanmar

Waislamu wasiopungua 150 wa jamii ya Rohingya wameuliwa katika mashambulio yaliyofanywa na jeshi la Myanmar katika eneo la Rakhine.

Asasi ijulikanayo kama Jumuiya ya Kitaifa ya Arakan ya Rohingya imetangaza kuwa ripoti kutoka eneo hilo zinaeleza kwamba kuanzia Jumamosi wiki hii hadi sasa Waislamu wasiopungua 150 wa jamii ya Rohingya wameuliwa katika mashambulio yaliyofanywa na jeshi huku serikali ya Myanmar ikijaribu kuzuia vyombo vya habari na makundi ya utoaji misaada yasifike katika eneo la Rakhine ili kuficha ukweli kuhusiana na mauaji hayo.

Serikali ya Myanmar imethibitisha kuuawa Waislamu wapatao 70 wa jamii ya Rohingya na wanajeshi 17 katika machafuko yaliyotokea siku chache zilizopita katika eneo la Rakhine.

Waislamu wa Myanmar wakilazimika kuhama makazi yao kunusuru maisha yao

Hatua kali za usalama zimechukuliwa kaskazini mwa eneo la Rakhine tangu tarehe 9 ya mwezi uliopita wa Oktoba, sambamba na kile kilichoelezwa kuwa shambulio dhidi ya askari wa mpakani ambapo askari polisi tisa waliuliwa.

Serikali ya Myanmar inawatuhumu Waislamu wa jamii ya Rohingya kuwa ndio waliofanya shambulio hilo huku ripoti rasmi zikieleza kwamba makumi ya watu wameuliwa na kutiwa nguvuni katika msako wa jeshi wa kuwatafuta wahusika wa mauaji hayo.

Wakaazi wa eneo la Rakhine na wanaharakati wa haki za binadamu wanaeleza kuwa katika mashambulio ya vikosi vya serikali jinai mbalimbali zinafanywa dhidi ya raia ikiwemo kuua watu bila ya sababu, ubakaji na kuchoma moto nyumba zao.

Waislamu wa Myanmar wamekuwa daima wakikabiliwa na mateso na unyanyasaji wanaofanyiwa na mabudha wanaoungwa mkono na serikali, lakini ukatili na mateso makubwa zaidi yamekuwa yakiwaandamana Waislamu wa jamii ya wachache ya kabila la Rohingya wanaoishi katika eneo la Rakhine.../