Mwito wa Suu Kyi wa umoja wa kitafa nchini Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i20569-mwito_wa_suu_kyi_wa_umoja_wa_kitafa_nchini_myanmar
Aung San Suu Kyi, Waziri wa Mambo ya Nje na mshauri mkuu wa serikali ya Myanmar ametaka kurejeshwa umoja wa kitaifa nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 02, 2016 03:01 UTC
  • Aung San Suu Kyi, Waziri wa Mambo ya Nje na Mkuu wa chama tawala nchini Myanmar
    Aung San Suu Kyi, Waziri wa Mambo ya Nje na Mkuu wa chama tawala nchini Myanmar

Aung San Suu Kyi, Waziri wa Mambo ya Nje na mshauri mkuu wa serikali ya Myanmar ametaka kurejeshwa umoja wa kitaifa nchini humo.

Amesema hayo mbele ya waajiri wa mashirika binafsi nchini Singapore na huku akikwepa kugusia jinai kubwa wanayofanyiwa Waislamu wa Rohingya na serikali ya chama chake katika mkoa wa Rakhine wa maghribi mwa Myanmar, amesisitiza kuwa, raia wa Myanmar ambao ni wa kaumu na makabila ya kila namna wanahitajia kuwa na utulivu ili kuvutia uwekezaji wa kigeni na jambo hilo muhimu haliwezekani bila ya kuweko utawala wa sheria nchini humo. Amesisitiza kuwa, serikali ya Myanmar haifurahishwi na hali ya machafuko iliyoko nchini humo hivyo inalihesabu suala la kuweko amani na umoja wa kitaifa kwa watu wote nchini humo, kuwa ni suala muhimu sana.

Watoto hawa Waislamu wa Myanmar wananyimwa hata haki yao ya kupata elimu kwa madai kuwa si raia wa nchi hiyo.

 

Kushiriki Waziri wa Mambo ya Nje wa Myanmar katika mkutano wa waajiri wa mashirika binafsi nchini Singapore kunaonesha namna anavyofanya juhudi za kuvutia uwekezaji wa kigeni kwa ajili ya kusaidia hali mbaya ya kiuchumi ya Myanmar na ameamua kutumia mbinu aina mbili kuwavutia wawekezaji, moja ni suala la utawala wa sheria na jengine ni umoja wa kitaifa. Ni jambo lisilo na shaka kuwa, mambo hayo yote mawili ni muhimu sana kwa serikali ya chama cha National League for Democracy cha Suu Kyi. Hata hivyo tatizo kubwa la Bi Suu Kyi na chama chake ni misimamo ya kindumilakuwili kuhusiana na mambo hayo mawili.

Hivi sasa jinai zinazofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu zimeiharibia jina mno nchi hiyo. Katika miaka ya hivi karibuni, Myanmar imekumbwa na matatizo mbalimbali ya kikaumu. Ukiachilia mbali jinai wanazofanyiwa Waislamu na serikali ya kibudha ya nchi hiyo, kaumu nyingine kama ile ya Kachine pamoja na uasi wa hivi karibuni wa watu wenye asili ya China katika mpaka wa nchi hiyo, umezitumbukiza katika mzozo nchi mbili jirani za Myanmar na China. Mara baada ya kuundwa serikali inayoonekana ya kirais huko Myanmar, Bi Suu Kyi alianza kuzungumzia suala la umoja na mshikamano wa watu wa jamii zote na wakati huo huo China nayo ikasema, iko tayari kuisaidia Myanmar kuzima uasi wa kundi la jamii ya wachache wenye asili ya China katika mpaka wa nchi hizo mbili wanaojulikana kwa jina la jeshi la Kokang.

Waokoeni Waislamu wa Rohingya

 

Hata hivyo kama tulivyotangulia kusema, mgogoro mkubwa wa Myanmar na ambao Bi Suu Kyi anajaribu kuukwepa kadiri anavyoweza, ni jinai wanazofanyiwa Waislamu wa nchi hiyo ambao wananyimwa hata haki zao za chini kabisa, yaani haki ya uraia. Mbali na kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bi Suu Kyi ndiye mkuu wa chama tawala cha National League for Democracy na anahesabiwa kuwa ndiye mpangaji mkuu wa sera na mambo yote yanayofanywa na serikali ya nchi hiyo. Kwa mtazamo wa wananchi wa Myanmar, kama kweli Bi Suu Kyi ana nia ya kweli ya kuimarisha utawala wa sheria na kuleta utulivu nchini Myanmaar, anapaswa achukue hatua za kivitendo za kuwatia mbaroni wahusika wa mauaji ya Waislamu wa Rohingya kama hatua ya awali ya kuleta utulivu na kuimarisha umoja wa kitaifa nchini Myanmar.