Kofi Annan yuko Myanmar kuchunguza ukatili dhidi ya Waislamu
Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan yuko nchini Myanmar kuchunguza ukatili wa jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya.
Annan na timu yake waliwasili Ijumaa katika Jimbo la Rakhine, eneo ambalo wiki iliyopita jeshi liliwaua Waislamu 86, kwa mujibu wa takwimu za serikali. Wachunguzi huru wanasema Waislamu zaidi ya 400 waliuawa kiholela.
Annan ameteuliwa na kiongozi asiye rasmi wa Myanmar Aung San Suu Kyi kuchunguza mauaji ya Waislamu wa Rohingya.
Suu Kyi ambaye anapigiwa debe na nchi za Magharibi kuwa eti ni 'nembo ya demokrasia' amelaumiwa vikali kwa kutochukua hatua yoyote ya maana kuwalinda Waislamu wa Rohingya ambao mashirika ya haki za binadamu yanasema wanaangamizwa kwa umati na jeshi.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa Waislamu wa kabila la Rohingya ni jamii ya wachache duniani inayodhulumiwa na kunyongeshwa zaidi. Serikali ya Myanmar inakataa kuwapa haki za uraia Waislamu ambao idadi yao ni zaidi ya watu milioni moja na laki tatu.
Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Thailand, Malaysia na Indonesia kutokana na mashambulio ya Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.