Der Spiegel: Waislamu wa Myanmar wanaendelea kuuawa kikatili
Gazeti mashuhuri la Ujerumani la Der Spiegel limeripoti kuwa, Waislamu wa Myanmar wanaendelea kukandamizwa kwa mbinu za kikatili.
Kwa kutegemea uchunguzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha Harvard cha Marekani, Der Spiegel limeripoti kuwa, hali ya Waislamu nchini Myanmar ni mbaya sana na kwamba, ni aina fulani ya mauaji ya kimbari.
Ripoti hiyo imesema kuwa, ukatili unaofanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu unatia wasiwasi na kwamba, kwa miaka mingi sasa kunafanyika mauaji ya siri ya kimbari nchini humo dhidi ya Waislamu.
Gazeti la Der Spiegel la Ujerumani limesisitiza kuwa, Waislamu wa Myanmar wamekuwa wakikabiliwa na tishio la njaa, maradhi na matatizo mengine ya kiafya kwa miaka mingi. Ripoti hiyo imesema jumuiya za misaada ya kibinadamu pia haziwasaidii Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar ambao limesema wanazingirwa na jeshi la nchi hiyo.
Maelfu ya Waislamu nchini Myanmar wameuawa na malaki ya wengine wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na mabudha wenye misimamo mikali wakisaidiwa na jeshi la nchi hiyo.