Mashambulio ya kutumia silaha moto yakithiri nchini Marekani
Kituo cha takwimu za mashambulio ya utumiaji bunduki nchini Marekani imetangaza kuwa katika muda wa masaa 48 yaliyopita matukio 190 ya mashambulio ya ufyatuaji risasi yameripotiwa nchini humo ambapo watu wasiopungua 61 wameuawa na wengine 116 wamejeruhiwa.
Tangu ulipoanza mwaka uliomalizika wa 2016 hadi tarehe 29 ya mwezi uliopita wa Desemba jumla ya matukio 57,371 ya ufyatuaji risasi yameripotiwa katika maeneo mbalimbali ya Marekani ambayo yalisababisha watu 14,859 kuuawa na wengine 30,315 kujeruhiwa.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, kati ya watu waliouawa, 662 ni watoto wenye umri chini ya miaka 11. Aidha tangu ulipoanza mwaka uliomalizika wa 2016 hadi sasa askari polisi wasiopungua 135 wameuawa wakiwa kazini, idadi ambayo ni ongezeko la asilimia 56 kulinganisha na mwaka 2015.
Gazeti la Washington Times limeandika kupitia ripoti maalumu kuwa, kwa wastani watu 88 hupoteza maisha kila siku nchini Marekani katika matukio ya utumiaji silaha moto yakiwemo ya watu wanaojiua. Hivi sasa utumiaji bunduki wa raia nchini Marekani umekuwa haudhibitiki tena na umekuwa tishio kwa maisha ya watu.
Baadhi ya watetezi wa uhuru wa kumiliki silaha wanalitaja suala hilo kuwa ni haki ya dhati ya mtu na sehemu ya msingi ya historia na turathi za Marekani…/