OIC kujadili mauaji na ukaandamizaji dhidi ya Waislamu wa Rohingya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i23296-oic_kujadili_mauaji_na_ukaandamizaji_dhidi_ya_waislamu_wa_rohingya
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) inatazamiwa kufanya mkutano wa kujadili mauaji na ukandamizaji wanaofanyiwa Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 12, 2017 03:47 UTC
  • OIC kujadili mauaji na ukaandamizaji dhidi ya Waislamu wa Rohingya

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) inatazamiwa kufanya mkutano wa kujadili mauaji na ukandamizaji wanaofanyiwa Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar.

Habari zinasema kuwa, Najib Razak, Waziri Mkuu wa Malaysia ndiye anayetazamiwa kuwa mwenyekiti wa mkutano huo wa OIC unaotazamiwa kufanyika wiki ijayo mjini Kuala Lumpur.

Wawakilishi 56 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushrikiano wa Kiislamu OIC wanatazamiwa kushiriki mkutano huo utakaofanyika Januari 19.

Nembo ya OIC

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa unafanya uchunguzi kuhusiana na ukandamizaji na mauaji yanayoripotiwa kufanywa dhidi ya jamii ya walio wachache ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar, ukandamizaji unaofanywa na jeshi la nchi hiyo likishirikiana na Mabudha wenye misimamo mikali.

Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Javad Zarif alimwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres akitaka umoja huo uzingatie zaidi hali mbaya ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wanaoteswa na kuangamizwa nchini Myanmar.

Tangu mwaka 2012 Mabudha wenye misimamo mikali wakisaidiwa na maafisa usalama wa Myanmar wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za ukatili, mauaji na hata kubaka wanawake Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo.

Ukatili dhidi ya watoto wa Rohingya

Serikali ya Myanmar imekataa kuwapa uraia Waislamu wa jamii ya Rohingya wapatao milioni 1.1 na kuwataja kama wahamiaji haramu kutoka Bangladesh.