Watu zaidi ya 30 wapoteza maisha katika ajali ya treni India
https://parstoday.ir/sw/news/world-i24052-watu_zaidi_ya_30_wapoteza_maisha_katika_ajali_ya_treni_india
Makumi ya watu wamepoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa katika ajali mbaya ya treni iliyotokea jana jioni kusini mashariki mwa India.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 22, 2017 04:48 UTC
  • Watu zaidi ya 30 wapoteza maisha katika ajali ya treni India

Makumi ya watu wamepoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa katika ajali mbaya ya treni iliyotokea jana jioni kusini mashariki mwa India.

Taarifa ya Shirika la Reli eneo la mashariki mwa nchi imesema kuwa, ajali hiyo ilitokea baada ya treni ya shirika la Jagdalpur-Bhubaneswar Express kuacha reli na kupinduka karibu na kituo cha Kuneru, wilaya ya Vizianagram, jimbo la Andhra Pradesh.

Habari zaidi zinasema kuwa, kwa akali watu 36 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 100 wakijeruhiwa katika ajali hiyo ya garimoshi. Mwezi Novemba mwaka uliopita, watu 90 walipoteza maisha baada ya garimoshi la abiria kuacha reli katika eneo la Pukhrayan, karibu na wilaya ya Kanpur Dehat, jimbo la kaskazini la Uttar Pradesh, kaskazini mwa India.

Kabla ya hapo, watu wengine 40 waliaga dunia na wengine 150 kujeruhiwa katika ajali nyingine ya treni katika jimbo la Uttar Pradesh. Ajali za garimoshi zimekuwa zikiripotiwa mara kwa mara nchini India, taifa ambalo watu milioni 23 hutumia usafiri wa reli kila siku.