Uingereza yabadili siasa zake kuhusu Syria na Rais Bashar Assad
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza amekiri katika Kamati ya Masuala ya Kigeni ya Bunge la nchi hiyo kwamba London imebadili siasa zake kuhusiana na Syria.
Boris Johnson amesema kuwa, London imekubali kwamba iwapo amani itarejeshwa nchini Syria, Rais Bashar Assad wa nchi hiyo anapaswa kuruhusiwa kushiriki tena katika uchaguzi wa rais.
Johnson amesema, kwa muda mrefu Uingereza imekuwa ikisisitiza kwamba Assad anapaswa kuondoka madarakani lakini imeshindwa kutekeleza suala hilo, na msimamo huo umeisababishia matatizo mengi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza amesema, suala muhimu ni kwamba serikali ya Rais Donald Trump huko Marekani pia inapaswa kukubali kwamba makubaliano yoyote na Russia kwa ajili ya kukomesha mgogoro wa Syria yanapaswa kuoana na matakwa na misimamo ya Iran ambayo ni mshirika mwingine mkubwa wa Syria.
Matamshi hayo ya Boris Johnson yanapingana kikamilifu na siasa za Uingereza ambayo tangu mwanzoni mwa vita vya Syria hadi sasa imekuwa ikisisitiza ulazima wa Rais Bashar Assad kuondoka madarakani.