Viongozi wa Myanmar wazuia uchunguzi kuhusu jinai dhidi ya Waislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i24379-viongozi_wa_myanmar_wazuia_uchunguzi_kuhusu_jinai_dhidi_ya_waislamu
Viongozi wa serikali ya Myanmar wamewazuia waandishi wa habari na waangalizi wa asasi kadhaa za kimataifa kufanya safari katika mkoa wa Rakhine ambao kwa miezi kadhaa umeshuhudia machafuko na ukatili mkubwa dhidi ya jamii ya Waislamu wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 29, 2017 03:52 UTC
  • Viongozi wa Myanmar wazuia uchunguzi kuhusu jinai dhidi ya Waislamu

Viongozi wa serikali ya Myanmar wamewazuia waandishi wa habari na waangalizi wa asasi kadhaa za kimataifa kufanya safari katika mkoa wa Rakhine ambao kwa miezi kadhaa umeshuhudia machafuko na ukatili mkubwa dhidi ya jamii ya Waislamu wa nchi hiyo.

Hii ni katika hali ambayo askari usalama wa Myanmar wanatuhumiwa kuhusika moja kwa moja katika jinai dhidi ya Waislamu wa mkoa huo na ripoti kuhusiana na suala hilo imepangwa kutangazwa hivi karibuni kupitia kamisheni ya uchunguzi ambayo iliundwa na serikali kwa ajili ya shughuli hiyo. Hata hivyo baada ya timu ya waandishi wa habari kuwasili katika mkoa wa Rakhine, viongozi wa eneo hilo waliwaambia kuwa, hakutakuwa na safari kuelekea maeneo yaliyokumbwa na machafuko hayo.

Askari katili wa Myanmar wanaohusishwa na ubakaji dhidi ya wanawake wa Kiislamu

Hivi karibuni kulisambaa picha za ukatili wa kijinsia unaowahusisha askari wa Myanmar wakiwabaka makumi ya wanawake wa Kiislamu wa mkoa huo na kadhalika picha za makumi ya miili ya Waislamu waliouawa na askari hao. Ukatili huo ulikuwa mkubwa kiasi cha kuwafanya hata baadhi ya askari kushindwa kuvumilia na hivyo kuamua kueneza video na picha zinazoonyesha askari hao wakipiga na kuwanajisi wanawake wa Kiislamu wa kabila la Rohingya.

Sehemu ndogo tu ya wanawake wa Kiislamu walionajisiwa na askari wa nchi hiyo

Kufuatia hali hiyo na kutokana na mashinikizo mbalimbali ya jamii ya kimataifa, hatimaye serikali ya Naypyidaw iliamua kuunda kamati ya uchunguzi ambayo ilitakiwa kuwasilisha ripoti yake mwishoni mwa mwezi huu wa Januari. Weledi wa mambo wameitaja hatua ya serikali ya nchi hiyo ya kuunda kamati hiyo kuwa ni kujaribu kujisafisha na ukatili wa askari hao.

Wanawake wa Kiislamu wa kabila la Rohingya

Kwa mujibu wa duru za habari mashambulizi ya hivi karibuni ya Mabudha dhidi ya Waislamu hao kwa akali yemepelekea watu elfu 66 wa kabila la Rohingya kukimbilia usalama wao nchini Bangladesh.