Kuongezeka wasiwasi wa kushadidi mgogoro wa wakimbizi Waislamu wa Myanmar
Hivi sasa ni jambo lililo wazi kwa kila asasi na jumuiya yoyote ya kimataifa kwamba, kuyapatia ufumbuzi matatizo ya Waislamu wa Myanmar si jambo la ndani bali ni kadhia ya kimataifa.
Kundi la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limesema katika ripoti yake kwamba, mashinikizo ya serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya yangali yanaendelea katika nchi hiyo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo ni kuwa, kuanzia mwezi Oktoba mwaka jana hadi sasa, jumla ya Waislamu 87,000 wa jamii ya Rohingya wamelazimika kuondoka katika makazi yao, sehemu zao za kazi na katika mashamba yao.
Jeshi la Myanmar linatajwa kuwa limekuwa na nafasi kubwa katika kutekeleza vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya. Hata hivyo inapasa kusema kuwa, serikali ya Myanmar nayo imekuwa na nafasi kubwa katika kutekeleza mauaji ya kizazi ikisaidiwa na Mabudha wenye misimamo ya kupindukia dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wanaopatikana katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa nchi hiyo.
Kwa hakika jambo hilo si geni tena kwa asasi yoyote ile ya kutetea haki za binadamu, Umoja wa Mataifa au Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC. Huenda serikali ya Bangladesh nayo ikatupiwa lawama kutokana na baadhi ya hatua inazochukua mipakani ambazo zinakwenda sambamba na matakwa ya serikali ya Myanmar katika kuwakandamiza maelfu ya wakimbizi wa Kirohingya, lakini endapo uhakika wa mambo utazingatiwa, Bangladesh ni nchi yenye wakazi wengi, iliyo nyuma kimaendeleo na inayokabiliwa na mapungufu mengi. Hivyo basi nchi kama hiyo inayokabiliwa na umasikini na matatizo ya kiuchumi haiwezi kutarajiwa kuwa mwenyeji mzuri wa maelfu ya Waislamu wa Myanmar wanaokimbia hujuma dhidi yao katika nchi yao.
Pamoja na hayo, Bangladesh kwa mtazamo wa fikra za waliowengi inahesabiwa kuwa nchi iliyo na jukumu na masuuliya katika hilo kwa kiwango cha uwezo wake wa kisiasa na kuwa kwake nchi ya Kiislamu. Licha ya kuwa katika maeneo ya kaskazini mwa Myanmar misaada ya Umoja wa Mataifa inaendelea kupelekewa Waislamu wa jamii ya Rohingya, lakini inaonekana kuwa, taasisi hii ya kimataifa haina uwezo unaotakiwa na wa kutosha kwa ajili ya kutekeleza majukumu; kwani haiwezi kuiambia serikali ya Myamnar iache kuweka vizingiti katika njia ya kuwafikishia misaada ya kibinadamu Waislamu hao.
Jumuiya za kiraia, Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC zina wasiwasi mkubwa kutokana na kuongezeka vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu wasio na ulinzi wa Myanmar. Kwa upande wake Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imetangaza kuwa, utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu ni mauaji ya kizazi.
Hamid al-Bar, mjumbe maalumu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC nchini Myanmar amesema kuwa, jumuiya hiyo inapaswa kuchukua hatua za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Myanmar ambao sasa sio suala la ndani bali ni kadhia ya kimataifa. Matamashi haya pamoja na misimamo ya maafisa wa OIC kuhusiana na kadhia ya Waislamu wa Myanmar inatolewa katika hali ambayo, kabla ya hapo, jamii ya kimataifa ilishuhudia mauaji ya kimbari katika nchi za Cambodia na Rwanda, ambapo jamii ya kimataifa ilikuwa mtazamaji tu wa mauaji hayo ya kizazi.
Bila shaka ni mahala pake sasa kwa nchi 57 wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kando ya Umoja wa Mataifa kutumia suhula na uwezo wao maalumu kwa ajili ya kuishinikiza serikali ya Myanmar ili isitishe mauaji na utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya. Hili ndilo tarajio pekee la Waislamu ulimwengu kutoka kwa taasisi hiyo ya kimataifa.