UN yataka Myanmar ikomeshe mauaji dhidi ya Waislamu
Ripoti ya Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema, mamia ya Waislamu wa kabila la Rohingya wameuawa nchini Myanmar katika ukandamizaji wa miezi ya hivi karibuni kwa kile kinachoonekana ni mauaji ya kimbari.
Katika taarifa iliyotoelewa leo Ijumaa, Zeid bin Ra’ad al-Hussein, Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema, vikosi vya usalama nchini Myanmar vimefanya mauaji ya umati, kuwabaka kwa pamoja Waislamu na kuteketezwa vijiji vyao katika kampeni mpya ya ukandamizaji iliyoanza mwezi Oktoba mwaka jana.
Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa wamerekodi vitendo vipya ya ukatili ikiwa ni pamoja na mateso, utekaji nyara, ubakakji wa kigenge na mauaji ya watoto wachanga hata wa miezi minane, vitendo viovu ambavyo vimefanywa na jeshi la Myanmar.
"Serikali ya Myanmar inapaswa kukomesha mara moja ukiukwaji huu mkubwa wa haki za binadamu za raia wake," amesema Hussein.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ametangaza ripoti hiyo baada ya Myanmar kuzuia maafisa wa umoja huo kuingia katika jimbo la Rakhine ambalo ni makao ya Waislamu wa kabila la Rohingya.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa, Waislamu wa Rohingya 65,000 ambao wamekimbia mchafuko ya hivi karibuni huko Myanmar, hivi sasa wanaishi kwenye kambi za wakimbizi nchini Bangladesh.
Halikadhalika Mabudha wanaounda asilimia 53 ya jamii ya Myanmar ndio wahusika wakuu wa mauaji ya Waislamu wa kabila la Rohingya katika mkoa wa Rakhine.
Ukandamizaji huo ulipamba moto mwaka 2012 ambapo Mabudha hao wakisaidiwa na maafisa usalama wa Myanmar walitumia mbinu mbalimbali za ukatili, mauaji na hata kubaka wanawake Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo, mbali na kunyimwa uraia, Waislamu wa jamii ya Rohingya wapatao milioni 1.1. Umoja wa Mataifa umewataja Waislamu wa Myanmar kuwa jamii inayokandamizwa zaidi dunaini.