Polisi wa Myanmar waunda kamati ya kuchunguza kuteswa Waislamu
Baada ya kuongezeka mashinikizo makubwa ya kimataifa, hatimaye jeshi la polisi la Myanmar limetangaza nia yake ya kuwasaili na kuwachunguza maafisa wa polisi wanaodaiwa kuwanyanyasa na kuwatendea vitendo viovu Waislamu wa Rohingya.
Wizara ya mambo ya Ndani ya Myanmar imetoa tamko na kusema kuwa, uchunguzi huo utafanywa ndani ya jeshi la polisi ili kubaini iwapo maafisa wa polisi wamehusika katika operesheni za kuangamiza Waislamu na kuvunjwa haki za binadamu dhidi ya Waislamu hao wa Rohingya.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu kutoa ripoti na kuwatuhumu maafisa usalama wa Myanmar kufanya jinai na uangamizaji wa kizazi cha Waislamu nchini humo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, maafisa wa polisi wa Myanmar waliwapiga risasi Waislamu waliokuwa wanakimbia mateso na kuchoma moto kikamilifu baadhi ya vijiji vya Waislamu hao.
Jeshi la polisi la Myanmar lilisema jana Jumatatu kuwa, ripoti ya Umoja wa Mataifa imetoa tuhuma nzito za uvunjaji wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na kuwatuhumu maafisa wa kijeshi wa Myanmar kuwanajisi Waislamu wa Rohingya. Afisa mmoja wa ngazi za juu wa polisi wa Myanmar amesema, jeshi hilo limeamua kuunda kamati maalumu ya uchunguzi ili kufuatilia na hatimaye kutoa majibu ya ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa.
Jeshi la Myanmar lilianzisha wimbi jipya la mashambulizi makali dhidi ya Waislamu wa kaskazini mwa nchi hiyo tangu mwezi Oktoba mwaka jana baada ya kushambuliwa askari wa mpakani wa nchi hiyo. Serikali ya mabudha ya Myanmar inadai kuwa Waislamu wa Rohingya ndio walioshambulia wanajeshi hao wa serikali, tuhuma ambazo zimekanushwa vikali na Waislamu hao.