Mwanachuoni kipofu wa Misri afia gerezani nchini Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i25338-mwanachuoni_kipofu_wa_misri_afia_gerezani_nchini_marekani
Sheikh Omar Abdu Rahman, mwanachuoni mashuhuri asiye na uwezo wa kuona mzaliwa wa Misri amefariki dunia akiwa gerezani nchini Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 19, 2017 01:15 UTC
  • Mwanachuoni kipofu wa Misri afia gerezani nchini Marekani

Sheikh Omar Abdu Rahman, mwanachuoni mashuhuri asiye na uwezo wa kuona mzaliwa wa Misri amefariki dunia akiwa gerezani nchini Marekani.

Kwa mujibu wa Greg Norton, Msemaji wa Gereza la Kifederali la Butner jimboni North Carolina, msomi huyo wa Kiislamu aliyekuwa na umri wa miaka 78 amefariki dunia baada ya kuugua kisukari kwa muda mrefu.

Mwanachuoni huyu aliyetambulika kwa kupinga wazi wazi utawala wa Kizayuni wa Israel sambamba na kukosoa vikali tawala za kidikteta za marais wa zamani wa Misri, Anwar Sadat na Hosni Mubarak, alifungwa jela na kuteswa katika nchi yake ya Misri, kabla ya kuhamia Marekani mwaka 1990.

Sheikh Omar Abdul Rahman akizungumza na waandishi wa habari  Aprili, 1993

Msomi huyo alikuwa akitoa mihadhara na darsa mbali mbali huko Brooklyn, karibu na mji wa New York, hususan za kukashifu dhulma na ukandamizaji wanaofanyiwa Wapalestina na utawala katili wa Israel.

Oktoba mwaka 1995, Sheikh Abdul Rahman alihukumiwa kifungo cha maisha jela, kwa tuhuma za kutoa hotuba za kichochezi mbali na eti kupanga njama za kutekeleza mashambulizi ya kigaidi mwaka 1993, dhidi ya majengo kama vile World Trade Center, daraja kubwa mashuhuri la George Washington na barabara za chini ya ardhi za Lincoln na Holland mjini New York; madai ambayo aliyapinga vikali. 

Miongoni mwa shakhsia ambao wamewahi kutoa wito wa kuachiwa huru mwanachuoni huyo kipofu, ni Muhammad Morsi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri ambaye aling'olewa madarakani kupitia mapinduzi.