India: Mashambulizi ya kibaguzi dhidi ya raia wetu nchini Marekani hayakubaliki
https://parstoday.ir/sw/news/world-i26188-india_mashambulizi_ya_kibaguzi_dhidi_ya_raia_wetu_nchini_marekani_hayakubaliki
Waziri wa Mambo ya Ndani nchini India sambamba na kulaani mashambulizi ya kibaguzi dhidi ya raia wa nchi hiyo huko Marekani, amesema kuwa New Delhi itaendelea kuwalinda raia wake walioko nje ya nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 10, 2017 09:50 UTC
  • India: Mashambulizi ya kibaguzi dhidi ya raia wetu nchini Marekani hayakubaliki

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini India sambamba na kulaani mashambulizi ya kibaguzi dhidi ya raia wa nchi hiyo huko Marekani, amesema kuwa New Delhi itaendelea kuwalinda raia wake walioko nje ya nchi.

Rajnath singh ameyasema hayo katika bunge la India na kuongeza kuwa, serikali ya nchi hiyo itaanza kuchukua hatua za lazima kwa ajili ya kuwalinda raia wake walioko nje ya nchi.

Raia wa India wanaoishi nchini Marekani

Katika siku za hivi karibuni, vyama vya upinzani nchini India vililalamikia kimya cha serikali ya Narendra Modi, Waziri Mkuu wa nchi hiyo juu ya mashambulizi ya kibaguzi dhidi ya raia wa India huko Marekani. Wapinzani hao mbali na kukosoa kimya hicho cha serikali ya India, wamesema kuwa, hujuma hizo za kibaguzi dhidi ya Wahindi huko Marekani ni suala la kutia wasi wasi mkubwa. Aidha siku chache zilizopita Sushma Swaraj, Waziri wa Mambo ya Nje wa India alinukuliwa akisema kuwa, kumeanzishwa uchunguzi dhidi ya mauaji ya raia wa nchi hiyo waliyeuawa katika mazingira ya kutatanisha huko Marekani.

Sushma Swaraj, Waziri wa Mambo ya Nje wa India

Alkhamis ya wiki iliyopita, Harish Patel raia wa India mwenye umri wa miaka 43, aliuawa na watu wasiojulikana karibu na nyumba yake huko Marekani. Aidha siku moja baadaye, aliuawa raia mweingine wa nchi hiyo na watu wasiojulikana mjini Washington, na hivyo kuwafanya Wahindi waishio Marekani kupatwa na hali ya wasi wasi mkubwa. Hujuma na mashambulizi ya kibaguzi nchini Marekani dhidi ya wageni, yameshika kasi zaidi baada ya kuingia madarakani Rais Donald Trump wa nchi hiyo inayojinai kuwa mtetezi wa haki za binaadamu duniani.