Kuendelea mauaji ya Waislamu nchini Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i26368-kuendelea_mauaji_ya_waislamu_nchini_myanmar
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limeituhumu serikali na jeshi la Myanmar kwa kuhusika katika jinai dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 14, 2017 07:55 UTC
  • Kuendelea mauaji ya Waislamu nchini Myanmar

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limeituhumu serikali na jeshi la Myanmar kwa kuhusika katika jinai dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini humo.

Katika taarifa, HRW imesema wakuu wa serikali na maafisa wa kijeshi nchini Myanmar wanawaua kwa umati Waislamu nchini humo mbali na kutekeleza jinai zinginezo zilizo dhidi ya binadamu.

Shirika hilo limesema, idadi kubwa ya Waislamu wa Myanmar wanalazimika kukimbia nchi yao kwa ajili ya kuokoa maisha yao. Serikali ya nchi jirani ya Bangladesh inasema, Waislamu 70,000 Warohingya wameingia nchini humo tokea mwezi Oktoba mwaka jana, wakitokea Myanmar.

Ripoti hiyo imetangazwa wakati ambapo baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti habari ya kuongozeka ukatili, mauaji, na ubakaji wa Waislamu mikononi mwa jeshi la Myanmar. Ni kwa sababu hii ndio sababu masaibu wanayopitia Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar yakatajwa kuwa ni maangamizi au mauaji ya kimbari yaani genocide.

Waislamu Myanmar katika kambi ya wakimbizi

Kudhulumiwa na kuuawa kwa umati Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar katika mkoa wa Rakhine kunaendelea wakati ambapo serikali ya nchi hiyo inadai kuwa oparesheni za kijeshi zimemalizika katika mkoa huo.

Oparesheni ya Jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu ilishika kasi mwezi Okotoba mwaka jana kwa kisingizio cha kuwasaka watu wenye silaha waliodaiwa kufanya hujuma katika vituo vya mpakani nchini humo. Tokea ilipoanza operesheni hiyo ya kikatili na kinyama mkoani Rakhine, mashahidi wanasema wanajeshi wamewanajisi wanawake Waislamu, wameteketeza kwa moto nyumba zao na  kuwaangamiza kwa umati Waislamu hao. Ripoti za ukatili na unyama huo zimeumiza nyoyo za walimwengu hasa Waislamu ambao wamelaani sera za maangamizi ya kimbari ambazo zinatekelezwa na utawala wa  mabudha wa Myanmar.

Kuendelea mauaji na unyama wa jeshi la mabudha wa Mynamara dhidi ya Waislamu kunajiri wakati ambapo mshauri wa usalama wa taifa nchini humo amedai kuwa, kila kitu ni shwari na  eti Waislamu hawadhulimiwi tena. Serikali ya Myanmar inajaribu kuwahadaa walimwengu wakati ambapo ni jambo lililo wazi kuwa Waislamu nchini humo wanaendelea kutendewa ukatili usio na kifani katika mkoa wa Rakhine.

Ili kuficha ukweli kuhusu jinai zake, serikali ya Myanmar imewapiga marufuku au kuwawekea vizingiti waandishi habari na wawakilishi wa mashirika ya haki za binadamu wanaotaka kufika Rakhine. Kwa njia hiyo wakuu wa Myanmar wanataraji watawazuia walimwengu kupata habari za mauaji ya kimbari ya Waislamu katika nchi hiyo. Hivi sasa ripoti zilizochapishwa kuhusu hali ya mambo huko Rakhine zimetolewa na Waislamu waliotoraka Myanmar na kuingia nchi jirani hasa Bangladesh

Mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada Myanmar wanaongoza kampeni ya kuwaangamiza Waislamu

Waislamu wa Myanmar hawauawi na kuteswa tu na vikosi vya serikali, bali hata Mabuda wenye misimamo ya kufurutu ada nao pia, kwa himaya ya vikosi vya usalama, wamehusika katika uhasama na ukatili mkubwa dhidi ya Waislamu hao katika nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Asia.

Pamoja na kuwa walimwengu wamelalamika na kuonyesha hasira zao kuhusu mauaji ya umati na kudhulumiwa Waislamu wa Myanmar lakini Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halijaonyesha kuchukizwa na yanayojiri Myanmar. Hii ni katika hali ambayo ni jukumu la baraza hilo kulinda na kudumisha amani ya kimataifa.

Walimwengu wanataraji kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litachukua hatua za haraka  kuushurutisha utawala wa Myanmar usitishe kikamilifu na mara moja ukatili dhidi ya Waislamu. Mbali na hilo taasisi za kisheria duniani hasa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC inapaswa kuchukua hatua za kuwafikisha kizimbani wale wote wanaohusika na mauaji ya kimbari na jinai nyinginezo dhidi ya Waislamu wa Myanmar.