Wenye misimamo mikali washindwa katika uchaguzi wa bunge Uholanzi
Matokeo ya uchaguz wa bunge Uholanzi yanaonyesha kuwa wanasiasa wenye misimamo mikali wamepata pigo huku chama cha Waziri Mkuu kikipata ushindi.
Kwa mujibu wa matokeo ya awali chama cha PVV cha mwanasiasa mwenye misimamo mikali ya kibaguzi na chuki dhidi ya Uislamu, Geert Wilders , kimepata viti 20 huku chama cha VVD cha waziri mkuu wa sasa Mark Rutte kikiwa kimepata viti 33 katika Bunge la Uholanzi lenye viti 150. Pamoja na hayo chama chenye misimamo mikali kimepata viti vingi zaidi katika uchaguzi huu kwani hapo kabla kilikuwa na vitu 12 huku chama cha VVD cha waziri mkuu nacho kikionekana kupoteza umashuhuri kwani huko nyuma kilikuwa na viti 41.
Vyama vya Christian Democrats na Democrats vimepata viti 19 kila kimoja huku vyama vilivyosalia vya Kijani, Leba na Soshalisti vikinyakua viti vilivyosalia. Asilimia 81 ya wapiga kura wanaripotiwa kushiriki katika uchaguzi huo wa Jumatano na idadi hiyo imetajwa kuwa ya kihisotria. Chama cha PVV cha Widlers kilitarajia kupata wingi wa kura kutokana na mgogoro wa wakimbizi na wahajiri nchini humo. Aidha chama hicho chenye chuki dhidi ya wageni kilitarajia kuwavutia wapiga kura kutokana na ongozeko la vitendo vya ugaidi barani Ulaya jambo ambalo limepelekea kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu barani humo.
Wakuu wa chama hicho walitazamia kuwa, kuingia madarakani vyama vyenye misimamo ya mrengo wa kulia katika baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya hasa baada Uingereza kujitoa katika umoja huo, kungechochea chama hicho nacho kupata ushindi na kuweza kuunda serikali. Kuingia madarakni Donald Trump Marekani ambaye ni rais mwenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia kumetoa motisha kwa wanasiasa wenye misimamo mikali ya ubaguzi barani Ulaya. Hao ni wanasiasa wanaopinga wahajiri, wanaounga mkono kujitenga na Umoja wa Ulaya na wanaosisitiza kuhusu utaifa zaidi ya ushirikiano wa kimataifa katika sekta za siasa na uchumi. Kwa msingi huo chama cha PVV cha Wilders kilikuwa na matumaini sana ya kupata ushindi.
Pamoja na hayo, Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte kupitia chama chake cha VVD ameweza kueneza sera zenye kuashiria uhalisia wa mambo na kuwaonya Waholanzi kuhusu nara za kibaguzi za chama cha Wilders na kwa njia hio kuweza kuwavutia wapiga kura.
Kati ya ahadi ambazo Rutte alitoa katika kampeni zake ni kukabiliana na kile alichokitaja kuwa ni 'machipuo ya misimamo mikali' barani Ulaya. Katika upande wa pili msuguano mkali baina ya Uturuki na Uholanzi katika siku ya hivi karibuni na kusimam kidete Mark Rutte mbela ya matakwa ya Rais Reccep Tayyip Erdogan wa Uturuki ni jambo ambalo lilipelekea umashuhuri wake kupanda miongoni mwa Waholanzi na hivyo chama chake kupata ushindi katika uchaguzi. Kwa mujibu wa sheria za Uholanzi, chama ambacho kinapata viti vingi zaidi bungeni kinapewa jukumu la kuunda serikali. Hadi sasa haijabainika iwapo kutaundwa serikali ya mseto au la kwani chama kilichoshinda kitakuwa na muda wa wiki kadhaa kuchukua maamuzi kuhusu suala hilo.
Pamoja na hayo,uchaguzi wa Uholanzi ulikuwa na umuhimu mkubwa si kwa nchi hiyo pekee, bali kwa bara zima la Ulaya. Wakuu wa nchi nyingi barani humo walikuwa wanafuatilia kwa karibu matokeo ya uchaguzi wa Uholanzi kwani iwapo chama chenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia kingeshinda, jambo hilo lingekuwa na taathira mbaya maana yamkini ushindi huo ungekaririwa katika nchi zingine.
Kwa kushindwa wanasiasa wenye misimamo mikali Uholanzi, kuna matumaini pia kuwa wanasiasa wenye misimamo kama hiyo ya kufurutu ada nao pia watashindwa Ujerumani na Ufaransa, nchi ambazo zinatarajia kufanya chaguzi hivi karibuni.
Ni wa sababu hii ndio maana baada ya ushindi wa chama chake, waziri mkuu wa Uholanzi amesema kuwa, baada ya kujiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya na ushindi wa Trump nchini Marekani, Uholanzi imesema 'la' kwa misimamo mikali ya kufurutu ada. Inatarajiwa kuwa matokeo hayo ya uchaguzi Uholanzi yatakaririwa tena katika nchi zingine za Ulaya.