Mar 19, 2017 07:46 UTC
  • Maelfu waandamana London, Uingereza kulaani chuki dhidi ya Uislamu

Maelfu ya watu wamejitokeza mabarabarani katika mji mkuu wa Uingereza, London kushiriki maandamano ya kulaani chuki na uenezaji hofu dhidi ya Uislamu (Islamophobia) na ubaguzi wa rangi.

Katika maandamano hayo ya jana Jumamosi, waandamanaji walikusanyika katika Medani ya Bunge mjini London, kulaani chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu, ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wahajiri na wakimbizi nchini humo.

Maandamano hayo yalifanyika sambamba na maadhimisho ya Umoja wa Mataifa ya Siku ya Kupambana na Ubaguzi.

Baadhi ya waandamanaji katika mji mkuu wa Uingereza, London

Maelfu ya Waingereza walioshiriki maandamano hayo ya London wamekosoa vikali matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Theresa May, kwamba matatizo yanayoikumba Uingereza kwa sasa zikiwemo changamoto za kiusalama yamesababishwa na wageni.

Mwishoni mwa mwaka uliopita, Kamisheni ya Kiislamu ya Haki za Binadamu yenye makao yake mjini London iliandaa mkutano wa kujadili suala la uenezaji chuki dhidi ya Uislamu, ubaguzi wa rangi na vilevile sababu ya kuongezeka chuki na hofu juu ya Uislamu katika Ulimwengu wa Magharibi. 

Katika miaka ya karibuni, mbali na Uingereza, chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu na mashambulio ya mitaani dhidi ya Waislamu na wahajiri yameongezeka mno katika nchi zingine za Ulaya.

Tags