Waislamu Canada: Hujuma dhidi ya Waislamu zimeongezeka mara mbili zaidi
Baraza la Kitaifa la Waislamu nchini Canada, limeonya juu ya ongezeko la vitendo vya chuki dhidi ya dini ya Uislamu nchini humo.
Taarifa iliyotolewa na baraza hilo imelaani vitendo hivyo na kusema kuwa, idadi ya mashambulizi yaliyofanywa ndani ya kipindi cha miezi mitatu iliyopita kuwalenga Waislamu imeongezeka mara mbili zaidi mwaka huu ikilinganishwa na wakati kama huo mwaka jana 2016.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mashambulizi hayo dhidi ya Waislamu nchini Canada yanafanyika katika vituo vya mabasi hadi kuchomwa moto msikiti wa mjini Toronto, na kadhalika hujuma ya watu wenye silaha dhidi ya msikiti wa Quebec na mauaji ya watu waliokuwa wakifanya ibada ya Swala.
Baraza la Kitaifa la Waislamu nchini Canada limesema kuwa tangu miaka mitano iliyopita jinai kadhaa zinazotokana na chuki dhidi ya Uislamu zimekuwa zikiripotiwa na kwamba vitendo hivyo vimeongezeka mara mbili zaidi. Sehrish Amjad, kiongozi wa haki za binadamu katika baraza hilo la Waislamu nchini Canada amesema kuwa, ubaguzi wa kuchupa mipaka wa rais wa sasa wa Marekani Donald Trump, ndio chanzo cha kushadidi hujuma dhidi ya Waislamu.
Ikumbukwe kuwa, tarehe 29 Januari, gaidi mmoja Mkristo mwenye misimamo mikali ambaye pia ni muungaji mkono wa Rais Donald Trump wa Marekani, aliingia msikitini wakati wa Swala ya Isha huko Quebec, Canada na kuwaua kwa kuwafyatualia risasi Waislamu sita na kuwajeruhi wengine wengi.
Hii ni katika hali ambayo, kiwango cha hujuma na mashambulizi dhidi ya Waislamu, kimeendelea kushuhudiwa nchini Marekani na kuongezeka mara mbili zaidi ndani ya kipindi cha miezi mitatu iliyopita.