Uingereza kuanza mchakato wa kujiondoa EU
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May mnamo Machi 29 atatia saini nyaraka za kujiondoa rasmi nchi yake katika Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit.
Baada ya utiwaji saini huo kutaanza mchakato wa mazungumzo magumu ya miaka miwili kuhusu mapatano ya kibiashara baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya.
Uingereza ilijiunga na Umoja wa Ulaya miaka 40 iliyopita na miezi tisa iliyopita Waingireza walishiriki katika kura ya maoni na kuunga mkono kujiondoa katika umoja huo. Balozi wa Uingereza EU, Tim Barrow, leo Jumatatu amemfahamisha Rais wa umoja huo, Donld Tusk kuwa nchi hiyo itatumia kipengee nambari 50 cha Mapatano ya Lisbon ambacho kinaainisha namna ya kujiondoa nchi mwanachama. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa kipingee hicho kutumika.

Kuna wasiwasi kuwa Uingereza itapoteza hadhi yake kama kituo cha harakati za kifedha barani Ulaya. Halikadhalika muungano wa miaka 310 wa England na Scotland uko hatarini na hatima ya Ireland Kaskazini nayo ikiwa matatani. Majimbo hayo pamoja na Wales ndio yanayounda nchi ya Uingereza.