NATO yakiri, usalama wa Ulaya uko mashakamani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i26814-nato_yakiri_usalama_wa_ulaya_uko_mashakamani
Kamanda wa majeshi ya NATO barani Ulaya, Jenerali Curtis Scaparrotti amekiri kuwa bara hilo sasa limekuwa miongoni mwa maeneo hatari zaidi duniani.
(last modified 2026-01-14T11:42:18+00:00 )
Mar 25, 2017 02:24 UTC
  • NATO yakiri, usalama wa Ulaya uko mashakamani

Kamanda wa majeshi ya NATO barani Ulaya, Jenerali Curtis Scaparrotti amekiri kuwa bara hilo sasa limekuwa miongoni mwa maeneo hatari zaidi duniani.

Jenerali Scaparrotti ameyasema hayo baada ya shambulizi la kigaidi la Jumatano iliyopita katika Daraja la Westminster nje kidogo ya jengo la Bunge la Uingireza mjini London. Amesema shambulizi hilo ni kielelezo cha hali ya hatari katika bara la Ulaya ambalo linakabiliwa na changamoto mbili kubwa za kurejea magaidi kutoka Syria na maeneo mengine, na tishio la ndani la wafuasi wa kundi la kigaidi la Daesh. 

Japokuwa tumekuwa tukisikia tahadhari zinazotolewa na maafisa wa usalama wa nchi za Ulaya ikiwemo Polisi ya Ulaya (Interpol) kuhusu ongezeko la vitisho vya kigaidi barani humo, lakini matamshi ya Jenerali Curtis Scaparrotti ambaye ni afisa wa ngazi za juu wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Ulaya (NATO) kuhusu tishio hilo ni kielelezo cha tishio kubwa, hali isiyo na kawaida na usalama unaolegalega wa nchi wanachama. Tunaweza kusema kuwa, matamshi hayo ni ishara kwamba, katika mtazamo wa NATO, vitisho vya ugaidi sasa vimeondoka katika hali ya kuwa jambo dogo la kawaida na kuwa maudhui muhimu zaidi ya usalama ambayo inapaswa kupewa mazingatio maalumu.

Majeruhiwa wa shambulizi la Westminster, London

Kwa hakika mashambulizi ya kigaidi ya mara kwa mara na ya kukaririwa katika nchi mbalimbali za Ulaya na hasara kubwa za nafsi na mali zinazosababishwa na mashambulizi hayo si tu kwamba vimebadili dhana ya hapo awali kwamba eneo la Ulaya magharibi ndilo lenye kiwango cha juu cha amani na hali bora zaidi ya maisha, bali pia sasa watu wa nchi za Ulaya wenyewe wanakabiliana na hatari kubwa inayoweza kuchukua maisha yao wakati na mahala popote pale katika nchi za bara hilo. Vitisho hivyo, kama alivyosisitiza kamanda wa majeshi ya NATO barani Ulaya, vinatokana na mambo mawili. Kwanza ni raia wa nchi hizo wanachama wa makundi ya kigaidi wanaorejea nyumbani. Suala hilo linapata nguvu zaidi hasa kwa kutilia maanani kushindwa kwa makundi ya kigaidi na kitakfiri kama Daesh huko Iraq na Syria. Vilevile kwa kutilia maanani idadi kubwa ya raia wa nchi za Ulaya waliojiunga na makundi ya kigaidi na kitakfiri kama Daesh, hapana shaka kuwa, kurejea kwao barani humo kunazidisha tishio la usalama katika nchi za bara hilo. 

Awali ilisemwa kuwa karibu raia elfu 5 wa nchi za Ulaya wamejiunga na kundi la Daesh, lakini mwezi Januari mwaka huu wa 2017 Mwenyekiti wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani ulaya, Sebastian Kurz alisema kuwa karibu raia elfu kumi wa nchi za bara hilo wamekwenda katika nchi za Iraq na Syria wka ajili ya kujiunga na kundi la kigaidi la Daesh. Idadi hii kubwa ya magaidi wa kitakfiri inaonesha hatari kubwa inayozikabili nchi za Ulaya.

Raia wa nchi za Ulaya wanachama wa kundi la Daesh

Suala la pili ni kuongezeka tishio la kigaidi la wafuasi wa kundi la Daesh ndani ya nchi za Ulaya ambalo pia limeashiriwa na Jenerali Curtis Scaparrotti. Katika tishio la hivi karibuni kabisa, baada tu ya shambulizi la Westminster mjini London, kundi la kigaidi la Daesh lilitoa tangazo likisema kuwa ndilo lililofanya shambulizi hilo na kwamba London inapaswa kujitayarisha kwa mashambulizi mengine.

Katika upande mwingine makundi ya kigaidi yamebadilisha mbinu za kutekeleza mashambulizi na badala ya kufanya hujuma za kujilipua kwa mabomu, sasa yanatumia magari kugonga umati wa watu au silaha baridi kama visu na mashoka, vitu ambavyo vinapatikana kwa urahisi. Mashambulizi kama haya tayari yameshuhudiwa katika nchi za Ujerumani, Ufaransa na hili la juzi la London, nchini Uingereza.