UN yaitaka Myanmar iwaachie huru watoto wadogo wanaozuiliwa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i27516-un_yaitaka_myanmar_iwaachie_huru_watoto_wadogo_wanaozuiliwa
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umeitaka serikali ya Myanmar kuwaachia huru watoto wadogo wanaozuiliwa na vyombo vya usalama chini ya mazingira magumu katika jimbo la Rakhine.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 09, 2017 14:01 UTC
  • UN yaitaka Myanmar iwaachie huru watoto wadogo wanaozuiliwa

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umeitaka serikali ya Myanmar kuwaachia huru watoto wadogo wanaozuiliwa na vyombo vya usalama chini ya mazingira magumu katika jimbo la Rakhine.

Hayo yamesemwa na Justin Forsyth, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF baada ya kuitembelea nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Asia na kubainisha kuwa, makumi ya watoto wadogo wa kabila la Rohingya wanazuiliwa katika gereza la Buthidaung jimboni Rakhine.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, iwapo hatua za kuipatia ufumbuzi kadhia ya Myanmar hazitachukuliwa,  basi zimwi la jinai dhidi ya Waislamu walio wachache katika jimbo la Rakhine litarejea kuitafuna nchi hiyo katika siku zijazo.

UNICEF imemtaka Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama cha 'Umoja wa Kitaifa kwa ajili ya Demokrasia' nchini Myanmar kufanya juu chini kuhakikisha kuwa watoto wadogo wanaozuiliwa nchini humo wanaachiwa huru.

Watoto madhulumu wa Myanmar

Hii ni licha ya shakhsia huyo ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kujitokeza wazi wazi na kuikingia kifua serikali. Wiki iliyopita, alidai kuwa hakuna mauaji ya umati yaliyotokea katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi hiyo, alipohojiwa na kanali moja ya televisheni ya Uingereza.  

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa mwezi Februari mwaka huu, jeshi la Myanmar lilihusika moja kwa moja katika mauaji ya umati, ubakaji na ukatili wa kutisha dhidi ya jamii ya wachache wa kabila la Rohingya wakiwemo watoto na wanawake. Karibu Waislamu milioni moja na laki moja wa kabila hilo wanaishi katika mkoa huo chini ya ubaguzi mkubwa wa Mabudha wenye misimamo mikali.