Hujuma ya Marekani Syria inaweza sababisha vita vya nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i27608-hujuma_ya_marekani_syria_inaweza_sababisha_vita_vya_nyuklia
Mbunge mmoja nchini Russia amelaani vikali hujuma ya hivi karibuni ya Marekani nchini Syria na kuonya kuwa hujuma hiyo yamkini ikaibua vita vya nyuklia duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 11, 2017 00:56 UTC
  • Hujuma ya Marekani Syria inaweza sababisha vita vya nyuklia

Mbunge mmoja nchini Russia amelaani vikali hujuma ya hivi karibuni ya Marekani nchini Syria na kuonya kuwa hujuma hiyo yamkini ikaibua vita vya nyuklia duniani.

Mikhail Yemelyanov mjumbe katika Bunge la Russia, Duma, amesema kitendo cha Marekani kuihujumu Syria hakiihusu Syria tu kwani Russia inaiunga mkono serikali halali ya Syria na hivyo inahusika na mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu. Yemelyanov amebaini kuwa hujuma hiyo ya Markeani haikuwa tu dhidi ya Syria bali ilikuwa dhidi ya Russia.

Amesema kwa kuzingatia kuwa wakati Wamarkeani wakivurumisha makombora katika uwanja wa ndege za kivita Syria hawakujua iwapo raia wa Russia walikuwa hapo au la ni jambo kama hilo linaloweza kuibua hali kama ile ya 'Mgogoro wa Makombora Cuba' ambao ulikaribia kuitumbukiza dunia kaitka vita vya nyuklia.

Uwanja wa Ndege wa Shayrat wa Jeshi la Syria uliolengwa na Marekani

Mikhail Yemelyanov pia amesema ni urongo mtupu kudai kuwa eti serikali ya Syria ilihusika na utumizi wa kemikali za sumu katika mji wa Khan Shaykhun, ambapo watu karibu 80 walipoteza maisha Aprili 4.

Amesema kemikali za sumu ziliondolewa mikononi mwa serikali ya Syria kitambo sana na hata Wamarekani walisimamia zoezi hilo.

Siku ya Ijumaa manoari za kivita za Marekani zilizo katika Bahari ya Mediterranean zilivurumisha makombora 59 ya Tomahawk nchini Syria na kulenga uwanja wa ndege za kivita wa Shayrat katika mkoa wa Homs. Watu wasiopungua tisa wakiwemo watoto wanne waliuawa katika hujuma hiyo ambayo imelaaniwa vikali duniani.