Marufuku ya Trump dhidi ya Waislamu yaanza kutekelezwa Marekani
Amri ya Rais Donald Trump wa Marekani inayowapiga marufuku raia wa nchi sita zenye idadi kubwa ya Waislamu kuingia katika ardhi ya Marekani imeanza kutekelezwa usiku wa kuamkia leo licha ya upinzani mkubwa dhidi ya uamuzi huo.
Amri hiyo imawazuia Waislamu kutoka nchi za Iran, Libya, Somalia, Sudan, Syria na Yemen pamoja na wahajiri kutoka nchi zote dunia kuingia Marekani katika kipindi cha siku 90 zijazo.
Amri hiyo imeanza kutekekezwa baada ya Mahakama Kuu ya Marekani Jumatatu iliyopita kuiruhusu serikali ya Rais Donald Trump kutekeleza sehemu ya amri ya kuwazuia Waislamu wa nchi kadhaa kuingia katika ardhi ya nchi hiyo.
Kiongozi mbaguzi wa Marekani, Donald Trump alitoa amri hiyo miezi mitano iliyopita na kukabiliwa na upinzani mkubwa nje na ndani ya Marekani na hatimaye kusitishwa na mahakama za nchi hiyo zilizosisitiza kuwa, ni ya kibaguzi na kwamba inapingana na katiba ya nchi hiyo. Hata hivyo Mahakama Kuu ya Marekani imesitisha maamuzi ya mahakama nyingine za nchi hiyo na kuruhusu utekelezaje wake.
Sambamba na utekelezaji wa amri hiyo ya kibaguzi dhidi ya Waislamu na wahajiri ya Trump, makundi ya wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu wamekusanyika katika viwanja vya ndege katika majimbo mengi ya nchi hiyo wakipinga uamuzi huo.
Msemaji wa Wizara ya mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassemi amesema kuwa, uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ya Marekani dhidi ya Waislamu ni kielelezo cha mienendo ya kibaguzi ya serikali ya Washington dhidi ya Waislamu na mtazamo usio wa kiadilifu kuhusu wafuasi wa dini hiyo.