Kulaaniwa mashambulizi dhidi ya Waislamu nchini India
https://parstoday.ir/sw/news/world-i32068-kulaaniwa_mashambulizi_dhidi_ya_waislamu_nchini_india
Waziri Anayehusika na Masuala ya Jamii ya Walio Wachache katika serikali ya India amelaani mashambulizi dhidi ya Waislamu na jamii nyingine za raia wachache nchini humo na kueleza kuwa vitendo vya utumiaji mabavu na ukandamizaji dhidi ya jamii za wachache vinavyofanywa na makundi yenye misimamo mikali ni njama zenye lengo la kuzuia maendeleo ya India.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 21, 2017 03:49 UTC
  • Kulaaniwa  mashambulizi dhidi ya Waislamu nchini India

Waziri Anayehusika na Masuala ya Jamii ya Walio Wachache katika serikali ya India amelaani mashambulizi dhidi ya Waislamu na jamii nyingine za raia wachache nchini humo na kueleza kuwa vitendo vya utumiaji mabavu na ukandamizaji dhidi ya jamii za wachache vinavyofanywa na makundi yenye misimamo mikali ni njama zenye lengo la kuzuia maendeleo ya India.

Mukhtar Abbas Naqvi jana alikadhibisha kwamba chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) kinapuuza mashambulizi dhidi ya Waislamu na kueleza kuwa New Delhi haijakaa kimya mkabala na vitendo vya makundi yenye misimamo mikali. Naqvi aliyasema hayo jana katika hotuba yake bungeni. Waziri huyo wa India amelaani shambulio lililofanywa na Wahindu wenye misimamo ya kufurutu ada dhidi ya Waislamu kwa kisingizio cha kumlinda ng'ombe na kutahadharisha kuwa kuendelea mashambulizi kama hayo kutakuwa na taathira mbaya. 

Viongozi wa serikali ya kizalendo ya chama tawala cha BJP wamezidisha tahadhari zao kwa Wahindu wenye misimamo mikali baada ya hivi karibuni Mahakama Kuu ya India kuondoa marufuku ya kuchinja ng'ombe na kuuza nyama yake;  wakat huo huo imeitaka serikali ya Waziri Mkuu Narendra Mondi iheshimu takwa hilo. Pamoja na hayo yote baadhi ya pande nchini India zinaamini kuwa kushadidi mashambulizi ya Wahindu wenye misimamo mikali dhidi ya Waislamu kuna mfungamano na kuingia madarakani chama tawala cha BJP. 

Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India  

 

Qassim Rasool Elias Katibu Mkuu wa chama cha Welfare anasema: Tangu kushika hatamu za uongozi serikali ya Modi mwaka 2014 vitendo vya Wahindu wenye misimamo ya kuchupa mipaka na mashambulizi dhidi ya jamii za walio wachache na Waislamu huko India vimeongezeka; na inaonekana kuwa Waziri Mkuu anadhibitiwa na Wahindu hao wenye misimamo mikali. Amesema mashambulizi hayo dhidi ya Waislamu na jamii nyingine  za walio wachache yanachafua pakubwa sura ya India.  

Pamoja na hayo yote kuna masuala mawili yanayopasa kuzingatiwa hapa kuhusiana na suala hilo.  

La kwanza ni kuwa hivi karibuni Waziri Mkuu wa nchi hiyo Narendra Modi alizungumza kuhusu India ya kisasa na kusisitiza kuwa katika jamii kama hiyo masuala ya ubaguzi, hitilafu za kikabila, kikaumu na kimadhehebu hazina maana; na suala la pili ni matamshi ya Waziri wa Serikali ya India Anayehusika na Jamii za Walio Wachache kuhusu maendeleo ya nchi hiyo kwamba: Waislamu wanashambuliwa ili kukwamisha maendeleo ya India. Matamshi haya ya viongozi wa ngazi ya juu wa serikali ya India yanabainisha wazi kuwa chama tawala cha BJP kimetambua vyema kwamba ustawi wa upande mmoja wa India hauwezi kuwa jibu kwa matakwa ya jamii nzima ya nchi hiyo. Hii ni kwa sababu India inaundwa na kaumu, makabila na madhehebu tofauti ambazo huku zikiwa na maendeleo ya kiteknolojia wakati huo huo jamii hizo zinapaswa kuzidisha maelewano na ushirikiano wao sambamba na kuvumiliana ili kudhihirisha tasiwra ya India kimataifa kuwa ni nchi inayostawi na inayoweza kuaminika khususan  kwa wawekezaji. 

Pamoja na kuwa chama tawala cha India cha Bharatiya Janata (BJP) ni chama chenye misimamo ya wastani chenye mfungamano na harakati ya Wahindu wenye misimamo mikali ya RSS, lakini kuhusiana na mustakbali wa matukio ya India inaonekana kuwa kuna hitilafu kati ya mirengo hiyo miwili ya kisiasa na kimadhehebu. RSS inapigania kuwepo jamii ya aina moja huko India  na kuzifanya jamii nyingine za walio wachache kama vile Waislamu na Wakiristo ziikimbie nchi kufuatia vitendo vya mabavu na kufurutu ada vinavyotekelezwa na harakati hiyo. Hii ni katika hali ambayo chama cha Bharatiya Janata ambacho kinaoongoza serikali ya India kinafuatilia mpango  wa maendeleo na ustawi wa pande zote kwa ajili ya kudhamini usalama, kuleta maelewano na kuishi kwa amani kati ya watu wote nchini humo. Mbali na mpango huo, chama hicho kimetoa zingatio kwa uchaguzi ujao kuwa kinapasa kustafidi na kura za walio wachache khususan za Waislamu ili kuweza kushinda kwa mara nyingine tena. 

Wanachama wa Harakati ya Wahindu wa India wenye misimamo mikali (RSS)

Alla Kul haal jamii ya wananchi wa India inaundwa na kaumu na madhehebu mbalimbali ambao wamekuwa wakiishi kwa amani na maelewano; na uhuru na mafanikio ya nchi hiyo yametokana na ushirikiano na mshikamano wa kitaifa wa India. Kwa msingi huo mashambulizi yanayofanywa na Wahindu wenye misimamo ya kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu kwa kisingizio chochote kile yanaweza kuitumbukiza hatarini amani na umoja wa India. Ndio maana wananchi wa India wakavitaka vyombo vya mahakama na serikali yao kukabiliana vikali na wahusika wa mashambulizi hayo dhidi ya Waislamu. Hii ni kwa sababu inaonekana kuwa kutolewa mara kwa mara kwa taarifa na hotuba hakujakuwa na athari yoyote ya maana katika kukomesha mashambulizi hayo.