Korea Kaskazini yaionya Marekani, yasema itaishambulia kwa nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i32320-korea_kaskazini_yaionya_marekani_yasema_itaishambulia_kwa_nyuklia
Korea Kaskazini imetangaza kuwa, ikiwa Marekani itafanya kosa kuishambulia kwa nyuklia, basi itapata jibu kama hilo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 27, 2017 04:43 UTC
  • Korea Kaskazini yaionya Marekani, yasema itaishambulia kwa nyuklia

Korea Kaskazini imetangaza kuwa, ikiwa Marekani itafanya kosa kuishambulia kwa nyuklia, basi itapata jibu kama hilo.

Pak Yong-sik, mmoja wa wajumbe wa ngazi za juu wa jeshi la Korea Kaskazini ameyasema hayo katika kikao cha kumbukumbu ya kumalizika vita kati ya Korea Kusini na Korea Kaskazini na kuongeza kwa kusema: "Ikiwa maadui watajaribu kutushambulia kwa kutumia silaha za nyuklia, sisi pia hata bila ya kutoa onyo lolote, tutaishambulia Marekani kwa silaha za nyuklia."

Pak Yong-sik, katikati akiwa kando ya kiongozi wa Korea Kaskazini

Onyo la Pyongyang limetolewa katika hali ambayo kumekuwepo na baadhi ya ripoti zinazosema kuwa, kuna uwezekano Korea Kaskazini ikafanya jaribio lingine jipya la kombora la balestiki la mabara katika siku ya maadhimisho ya kumbukumbu za kuhitimishwa vita kati ya Korea mbili, yaani tarehe 27 Julai mwaka 1953. Viongozi wa Marekani wanasema kuwa, maandalizi ya shughuli za majaribio ya kombora hilo yamehamishiwa katika mji wa Kaesong, magharibi mwa Korea Kaskazini na kwamba maandalizi hayo yanaonyesha kwamba, Pyongyang inajiandaa kulifanyia majaribio kombora hilo la mabara. Tarehe nne mwezi huu Korea Kaskazini ililifanyia majaribio kombora la kwanza la kuvuka mabara ambapo ililiambatanisha na teknolojia ya kubeba kichwa cha nyuklia.

Moja ya makombora ya Korea Kaskazini yanayoitia kiwewe Marekani na washirika wake

Wakati huo huo, Baraza la wawakilishi la seneti nchini Marekani limepiga kura ya kuziwekea vikwazo vipya nchi tatu za Russia, Iran na Korea Kaskazini. Kwa mujibu wa kura hiyo, Russia imewekewa vikwazo hivyo kwa kile kinachodaiwa na Washington kuwa ni hatua ya Moscow ya kuingilia uchaguzi mkuu wa mwaka jana nchini Marekani, huku Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Korea Kaskazini zikiwekewa vikwazo hivyo kwa madai ya majaribio yao ya makombora.