Takwa la Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kwa Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i32674-takwa_la_jumuiya_ya_ushirikiano_wa_kiislamu_(oic)_kwa_myanmar
Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) Yusuf bin Ahmed Al-Othaimeen ameitaka serikali ya Myanmar kuheshimu haki za Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 04, 2017 06:48 UTC
  • Takwa la Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kwa Myanmar

Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) Yusuf bin Ahmed Al-Othaimeen ameitaka serikali ya Myanmar kuheshimu haki za Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo.

Akiwa katika safari ya siku nne huko Dhaka nchini Bangladesh, Al-Othaimeen amesisitiza kuwa, serikali ya Mnanmar inapaswa kuheshimu na kutambua rasmi haki za kiraia za Waislamu wa Rohingya.

Wito huo umetolewa baada ya Mabudha wenye misimamo mikali kufanya mashambulizi mapya dhidi ya kijiji cha Kaing Gyi katika mkoa wa Rakhine na kuua Waislamu kadhaa.

Yusuf bin Ahmed Al-Othaimeen

Tangu muongo wa 1960 serikali ya Myanmar ilianzisha mikakati kabambe ya kuwabinya na kuwashinikiza Waislamu wa jamii ya Rohingya ya nchi hiyo ili waache mashamba, nyumba na milki zao na kuondoka nchini humo. Mwaka 2012 serikali ya Myanmar ilizidisha mashinikizo ya kisiasa na kuchochea mashambulizi na mauaji ya Mabudha wenye misimamo mikali dhidi ya Waislamu hao. Serikali ya Mnanmar imewanyima Waislamu hao haki zote za kiraia na inasema wanapaswa kuondoka nchini humo na kwenda Bangladesh ambako inadai ndiko walikotoka. Hata hivyo madai hayo yanakadhibishwa na ukweli wa kihistoria unaothibitisha kuwa, Waislamu wa Rohingya wamekuwa wakiishi nchini Myanmar hususan katika ardhi ya Arakan yaani Rakhine ya sasa kwa karne kadhaa zilizopita na walikuwa na utawala wa kifalme katika jimbo hilo. Kwa msingi huo mashinikizo na mauaji yanayofanywa dhidi ya Waislamu wa Rohingya ni harakati ya kisiasa inayofanywa na mabudha kwa shabaha ya kuangamiza kizazi chao.

Waislamu wa jamii ya Rohungya

Salkom Ouglou ambaye ni mtaalamu wa Jumuiya ya Utafiti wa Statijia za Kimataifa ya Ankara nchini Uturuki anasema: "Tangu miaka kadhaa iliyopita serikali ya Myanmar ilianza kutekeleza sera za kuwafuta Waislamu wa Rohingya kwa shabaha ya kuasisi nchi yenye misingi ya Kibudha".  

Vilevile Muhmmad al Masery ambaye ni mtaalamu wa masuala ya eneo la kusini mashariki mwa Asia anasema: Kwa sasa Myanmar inashuhudia kipindi cha mauaji kamili ya kimbari kama yale yaliyotokea Bosnia Herzegovina katika muongo wa 1990 au yale yanayofanywa na Wazayuni wa Israel huko Palestina. Vilevile si jambo lililo mbali kwamba, kuna ushirikiano wa nyuma ya pazia baina ya Magharibi na serikali ya Wabudha wa Myanmar kuhusu kadhia ya Waislamu wa Rohingya", mwisho wa kunukuu.

Ili kupunguza mashinikizo ya kimataifa, serikali ya Myanmar imedai kuwa Waislamu wa Rohingya wanachoma moto nyumba zao wenyewe, madai ambayo yamepingwa na jumuiya zote za kimataifa. Ripota Maalumu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Yanghee Lee anasema: Madai yanayotolewa na serikali ya Myanmar kuwa Waislamu wa Rohingya wanachoma moto nyumba zao wenyewe si ya kweli, na mwenendo wa polisi ya Myanmar wa kuwapiga, kuwanyanyasa na kuwashambulia wanavijiji Waislamu sasa limekuwa jambo la kawaida".

Nyumba zao zinachomwa na wanawake wanabakwa na kunajisiwa

Jambo la kutiliwa maanani zaidi ni kuwa, jumuiya za kimataifa zinazodai kutetea haki za binadamu za Magharibi zimepuuza na kunyamazia kimya kabisa mauaji yanayofanywa na Mabudha wa Myanmar dhidi ya Waislamu wanaokandamizwa na hazifanyika jitihada za aina yoyote za kuilazimisha serikali ya nchi hiyo kutambua rasmi haki za kiraia za watu hao.

Alaa kulli hal, baadhi ya watawa wa Kibudha kama Ashin Wirathu ambaye ni kiongozi wa kidini na kiroho wa harakati ya kukabiliana na Waislamu nchini Myanmar, wameunda kundi linalojulikana kwa jina la 969 linalofanya mauaji ya kimbari na kizazi cha Waislamu wa Rohingya.

Kwa msingi huo na katika hali ya sasa ya kimya cha jamii ya kimataifa na jumuiya za kutetea haki za binadamu, inaonekana kuwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) itakuwa na kibarua kigumu sana cha kuwatetea Waislamu hao wanaoendelea kudhulumiwa na kuangamizwa.