Wamarekani waandamana kupinga ubaguzi katika jimbo la Utah
-
Waandamanaji wakichoma moto bendera ya makundi ya wabaguzi wa rangi, Marekani
Maelfu ya raia wa Marekani wamefanya maandamano wakipinga sera za kibaguzi za wazungu katika mji wa Salt Lake ambao ni makao makuu ya jimbo la Utah huko kusini mwa nchi hiyo.
Maafisa wa Jimbo la Utah wamesema lengo la maandamano hayo ambayo yamehudhuriwa pia na maafisa wa vyama viwili vya Democratic na Republican ni kulaani chuki za kibaguzi ambazo siku chache zilizopita zilisababisha ghasia na machafuko makubwa nchini Marekani.
Waandamanaji hao walikuwa na mabango yenye maandishi yanayopinga ubaguzi na sera za Rais Donald Trump wa Marekani.
Mbunge wa chama cha Republican katika Kongresi ya Marekani, Mia Love aliyehutubia waandamanaji ameashiria ukatili unaotokana na fikra na sera za kibaguzi nchini Marekani na kutoa wito wa kupambana na chuki za kibaguzi na kuwa na umoja na mshikamano baina ya watu wa mbari zote nchini humo.
Maandamano hayo yamefanyika baada ya machafuko ya Jumamosi iliyopita ambapo watu watatu waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Ghasia hizo zilitokea baada ya makundi ya wabaguzi wa rangi nchini Marekani kama yale ya Ku Klux Klan, neo-Nazis na skinheads kuvamia maandamano ya amani ya watetezi wa haki za binadamu wanaotaka masanamu ya vinara wa harakati za kibaguzi nchini humo yaondolewa katika maeneo mbalimbali ya miji ya Marekani.