Uchunguzi: Zaidi ya asilimia 30 ya Wafaransa wanaishi kwenye umasikini
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34373-uchunguzi_zaidi_ya_asilimia_30_ya_wafaransa_wanaishi_kwenye_umasikini
Uchunguzi uliofanywa nchini Ufaransa unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 30 ya raia wa nchi hiyo wanaishi kwenye umasikini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 15, 2017 03:23 UTC
  • Uchunguzi: Zaidi ya asilimia 30 ya Wafaransa wanaishi kwenye umasikini

Uchunguzi uliofanywa nchini Ufaransa unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 30 ya raia wa nchi hiyo wanaishi kwenye umasikini.

Shirika la Uchunguzi wa Maoni na Utafiti wa Masoko Duniani (IPSOS) limeeleza katika ripoti yake ya kila mwaka kuwa zaidi ya asilimia 30 kati ya Wafaransa wote milioni 67 wanaishi kwenye umasikini na wengine asilimia 20 wanakaribia mstari wa umasikini.

Ripoti ya mwaka huu ya shirika hilo inaonyesha kuwa asilimia 57 ya watu walioshiriki kwenye utafiti wa IPSOS wameeleza kwamba wanaihisi mno hatari ya umasikini katika maisha yao. Hii ni katika hali ambayo asilimia 55 ya waliotoa maoni yao katika uchunguzi wa mwaka uliopita wa 2016 walikuwa na hisia hiyo na asilimia 52 katika mwaka wa kabla yake wa 2015.

Masikini akitafuta chakula kwenye debe la taka

Isitoshe, kati ya kila Wafaransa watano, mmoja wao anaitakidi kwamba anakabiliwa na mashinikizo makubwa ili kuweza kujikimu mahitaji yake ya kila mwezi.

Aidha watu wanane kati ya 10 walioshiriki kwenye uchunguzi wa maoni uliofanywa na IPSOS wameeleza kuwa vijana ndio wanaokabiliwa zaidi na hatari ya kukumbwa na umasikini.

Uchunguzi huo umebainisha pia kwamba asilimia 39 ya waliyotoa maoni yao wamesema hawana uwezo wa kulipa gharama za matibabu.

Ripoti ya Shirika la Uchunguzi wa Maoni na Utafiti wa Masoko Duniani imeeleza kuwa takwimu hizo zinaonyesha wazi mbinyo na mashinikizo wanayokabiliana nayo wananchi wengi wa Ufaransa.../