Ufaransa yashangazwa na Trump kuzuia raia wa Chad kuingia Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34933-ufaransa_yashangazwa_na_trump_kuzuia_raia_wa_chad_kuingia_marekani
Serikali ya Ufaransa imekosoa vikali hatua ya Washington ya kuijumuisha Chad katika orodha ya nchi ambazo raia wake wamepigwa marufuku kuingia Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 27, 2017 22:58 UTC
  • Ufaransa yashangazwa na Trump kuzuia raia wa Chad kuingia Marekani

Serikali ya Ufaransa imekosoa vikali hatua ya Washington ya kuijumuisha Chad katika orodha ya nchi ambazo raia wake wamepigwa marufuku kuingia Marekani.

Agnes Romatet-Espagne, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Ufaransa aliyasema hayo jana Jumatano na kuongeza kuwa, nchi hiyo ya Ulaya imeshangazwa na hatua hiyo ya Marekani dhidi ya Chad, nchi ya Afrika ambayo Paris inaiona kama mshirika wake mkubwa katika vita dhidi ya ugaidi.

Sambamba na kuitaka Marekani iuangalie upya msimamo huo dhidi ya Chad, afisa huyo wa serikali ya Ufaransa amesema: "Chad ni mshirika mkubwa katika mapambano dhidi ya ugaidi, na tayari imeshalipa gharama kubwa katika vita hivyo."

Rais Donald Trump wa Marekani

Ifahamike kuwa, mji mkuu wa Chad, N‘djamena ni mwenyeji wa makao makuu ya kikosi cha Ufaransa chenye askari elfu nne cha kupambana na magenge ya kigaidi magharibi mwa Afrika. 

Hivi karibuni, Rais Donald Trump aliziongeza Korea Kaskazini, Chad na Venezuela katika orodha ya nchi ambazo raia wao hawaruhusiwi kufanya safari nchini Marekani. 

Nchi nyingine ni Iran, Syria, Libya, Somalia na Yemen, huku Sudan iliyokuwa katika orodha ya awali ikiondolewa katika orodha mpya.