Radiamali ya India baada ya kugunduliwa kaburi la umati nchini Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i35073-radiamali_ya_india_baada_ya_kugunduliwa_kaburi_la_umati_nchini_myanmar
Baada ya kutangazwa habari ya kugunduliwa kaburi la umati lenye idadi kubwa ya maiti za Waislamu wa jamii ya Rohingya katika mkoa wa Rakhine wa magharibi mwa Myanmar, serikali ya India imeonesha kusikitishwa sana na uhalifu huo na kutaka kupandishwa kizimbani wahalifu wote waliofanya jinai hiyo ya kutisha.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Oct 01, 2017 02:37 UTC
  • Waislamu wanakimbilia zaidi Bangladesh si India kutokana na uungaji mkono wa India kwa jinai dhidi ya Waislamu hao nchini Myanmar
    Waislamu wanakimbilia zaidi Bangladesh si India kutokana na uungaji mkono wa India kwa jinai dhidi ya Waislamu hao nchini Myanmar

Baada ya kutangazwa habari ya kugunduliwa kaburi la umati lenye idadi kubwa ya maiti za Waislamu wa jamii ya Rohingya katika mkoa wa Rakhine wa magharibi mwa Myanmar, serikali ya India imeonesha kusikitishwa sana na uhalifu huo na kutaka kupandishwa kizimbani wahalifu wote waliofanya jinai hiyo ya kutisha.

Rajiv Kumar, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya India amesema, nchi yake inalaani vikali vitendo vyote vya kigaidi na inataka ukatili na jinai zikomeshwe mara moja na wale wote waliohusika na jinai hizo watiwe mbaroni na kufikishwa mahakamani.

Watoto wadogo ndio wahanga wakubwa wa ugaidi wa mabudha nchini Yemen. Watoto wa Waislamu wa jamii ya Rohingya waliokufa maji wakati wakikimbia ukatili wanaofanyiwa nchini kwao 

 

Baada ya kushinikizwa sana na jamii ya kimataifa tena kwa muda mrefu, hatimaye siku chache zilizopita serikali ya Myanmar iliruhusu mashirika ya haki za binadamu kuingia katika mkoa wa Rakhine wa magharibi mwa nchi hiyo tab'an chini ya upekuzi na uangalizi mkali wa serikali. Katika hatua za awali kabisa wa kutembelea eneo hilo, mashirika hayo ya haki za binadamu yamegundua kaburi la umati lenye miili 28 ya Waislamu wa Rohingya, 20 kati yamiili hiyo ni ya wanawake na minane ni ya wanaume. Hapo serikali ya Myanmar imeshindwa kuficha habari hiyo.

Takwimu zinaonesha kuwa, tangu tarehe 25 Agosti mwaka huu wakati lilipoanza wimbi jipya la mauaji ya Waislamu huko magharibi mwa Myanmar hadi hivi sasa, mabudha na wanajeshi wa nchi hiyo wameshaua Waislamu zaidi ya elfu sita wa jamii ya Rohingya na kujeruhi wengine alfu nane.

Hisia kali za India kuhusu kugunduliwa kaburi hilo la umati lenye miili ya Waislamu kwenye jimbo la Rakhine la magharibi mwa Myanmar zimetolewa katika hali ambayo hadi sasa India imekuwa na msimamo tata kuhusiana na mauaji wanayofanyiwa Waislamu hao.

Mashirika yanayojigamba kutetea haki za binadamu yananyamazia kimya ukatili wanaofanyiwa Waislamu hawa wasio na ulinzi

 

Katika miezi ya hivi karibuni, India ilichukua hatua iliyoonekana ni ya kuunga mkono mauaji ya umati wanayofanyiwa Waislamu nchini Myanmar. Serikali ya New Delhi ilitoa amri ya kufukuzwa Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini India kwa madai eti wanahatarisha usalama wa nchi hiyo.

Kwa kweli hakuna sababu yoyote inayoweza kuhalalisha uamuzi huo wa India wa kuwafukuza Waislamu hao ambao wamekimbia kwao kutokana na ukatili na mauaji ya kinyama wanayofanyiwa na magaidi wa kibudha wenye chuki za kidini. India kama Bangladesh, inapakana na Myanmar, lakini Waislamu wa Rohingya wanajikubalisha kustahamili tabu nyingi kuhakikisha wanakimbilia zaidi Bangladesh kuliko India. Msimamo kama huo wa New Delhi unaweza kuwa sababu ya idadi kubwa ya Waislamu wa jamii ya Rohingya kukimbilia Bangladesh na si India.

Hata hivyo uamuzi wa serikali ya India wa kuwafukuza nchini humo maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya waliokimbia ukatili na mauaji huko Myanmar, umepokewa kwa hisia kali ndani ya India kwenyewe na pia kutoka kwa taasisi mbalimbali za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa.

Muislamu wa jamii ya Rohingya akishindwa kujizuia kulia kwa kuona ukatili waliofanyiwa jamaa zake na mabudha wakishirikiana na wanajeshi wa Myanmar

 

India haikutosheka na kunyamazia kimya na kutolaani jinai kubwa za kibinadamu zinazofanywa na mabudha na wanajeshi wa Myanmar dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo, bali imefika mbali zaidi na kuamua kuwafukuza maelfu ya wakimbizi Waislamu wanaokimbilia nchini humo. Hivi sasa lakini India imejitokeza na kuwalaani magaidi waliowaua Waislamu hao na kuwazika kwenye kaburi la umati huko Rakhine, Myanmar. Si hayo tu, lakini pia imetaka wahalifu waliotenda jinai hiyo watiwe mbaroni na wapandishwe kizimbani. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, msimamo huo wa hivi sasa wa India ni katika kujaribu kupunguza mashinikizo ya kimataifa dhidi yake, kutokana na kunyamazia kimya jinai wanazofanyiwa Waislamu huko Myanmar na uamuzi wake wa kuwafukuza nchini humo maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.

Hatua nyingine iliyochukuliwa na India ya kupunguza mashinikizo ya kimataifa dhidi yake ni uamuzi wake wa kujiunga katika tamko la Jumuiya ya Kimataifa ya Mabunge lililotolewa mjini Bali Indonesia ambalo limeilaani serikali ya Myanmar kwa kuruhusu jinai dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.

Hata hivyo hatua hizo za India hazitoshi hata kidogo, kwani New Delhi ina uhusiano mzuri na wa karibu na serikali ya Myanmar na inaweza kutumia ushawishi wake kuzuia ukatili na mauaji wanayofanyiwa Waislamu wa Myanmar na mabudha na wanajeshi ya nchi hiyo hususan mkoani Rakhine.