Wendy Sherman atetea tena makubaliano ya nyuklia ya Iran
Mwanadiplomasia wa zamani wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani amesema kuwa, uhusiano kati ya nchi hiyo na Korea ya Kaskazini utaharibika zaidi iwapo Rais wa nchi hiyo Donald Trump atakataa kuthibitisha kwamba Iran imeheshimu na kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Akizungumza huko New York, Wendy Sherman ameongeza kuwa, iwapo Rais Donald Trump hatothibitisha kuwa, Iran imeheshimu makubaliano hayo ya nyuklia na suala hilo kulikabidhi kwa Kongresi ya nchi hiyo, hatua hiyo itakuwa na taathira hasi.
Mwanadiplomasia huyo wa zamani wa Marekani am,ehoji kuwa iwapo Trump hatotangaza kuwa Iran imetekeleza majukumu yake kuhusu makubaliano hayo ya nyuklia, basi kwa nini Korea ya Kaskazini inapasa kufanya mazungumzo na Marekani?
Afisa huyo wa ngazi ya juu wa timu ya mazungumzo ya Marekani katika mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 ameashiria vitisho vya Rais wa nchi hiyo Donald Trump kwamba atakataa kuthibitisha kufungamana Iran na makubaliano ya JCPOA na akasema: Hatua ya kujizuia kuthibitisha kuwa Iran imetekeleza majukumu yake kuhusu makubaliano hayo itasababisha hali ya kutoaminiana.
Rais Donald Trump wa Marekani tarehe 12 mwezi huu anatazamiwa kutangaza uamuzi wake kuhusu makubaliano ya JCPOA na kuweka wazi stratejia kuu ya serikali yake kuhusu Iran.
Makubaliano ya nyuklia ya Iran na kundi la 5+1 linaloundwa na Uingereza, Ufaransa, Russia, Uchina, Marekani pamoja na Ujerumani mashuhuri kama JCPOA yalianza kutekeleza Januari mwaka jana. Hata hivyo serikali ya Marekani imekuwa ikikiuka utekelezaji wa makubaliano hayo ya kimataifa ikiwa moja ya nchi wanachama wa kundi hilo.