FBI yaonya kuhusu tishio la misimamo mikali ya Waafrika Wamarekani
Shirika la upelelezi la Marekani FBI limeonya kuhusu kile kinachodaiwa ni tishio la misimamo mikali ya Waafrika Wamarekani au Wamarekani weusi.
Jarida la Foreign Policy linasema limepokea waraka ulioandikwa Agosti 2017 na kitengo cha FBI cha ugaidi wa ndani ya nchi ambapo kadhia ya tishio la Wamarekani weusi imechunguzwa kwa kina.
FBI imeonya kuwa, ukatili wa polisi dhidi ya Waafrika Wamarekani umepelekea kuibuka misimamomikali miongoni mwa jamii hiyo nchini Marekani. Taarifa zinasema hivi sasa Wamarekani weusi wanajizatiti kwa silaha ili kutetea haki zao na kukabiliana na dhulma wanazotendewa.
Waraka huo umebaini kuwa, machafuko miongoni mwa Wamarekani weusi sasa yamechukua mkondo wa kiaidiolojia huku wengi wakiamini kuwa, lazima wajizatiti kwa silaha kwa ajili ya kujitetea.
Kachero wa zamani wa FBI, Michael German anasema hivi sasa polisi nchini Marekani wanaingiwa na kiwewe na wahka wanapokabiliana na Wamarekani weusi. Mwaka huu pekee Polisi ya Marekani imewapiga risasi kiholela watu 750 ambapo 170 walikuwa ni Waafrika Wamarekani.

Ripoti hiyo imesema tukio la mwaka 2014 la kupigwa risasi na kuuawa bila hatia kijana Michael Brown katika mji wa Ferguson jimboni Misouri na kuachiliwa huru afisa aliyehusika na mauaji hayo ya kinyama ndio chimbuko la harakati mpya ya Wamarekani Weusi ijulikanayo kama Black Identity Extremist (BIE).
Wakati huo huo matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na taasisi ya Forward Institute yanaonesha kuwa, thuluthi mbili ya vijana wa Marekani wenye asili ya Afrika na karibu nusu ya Malatino wamekumbana na maudhi na ukatili wa polisi ya nchi hiyo.