Comey: Trump ni kidhabi, ameichafua taswira ya FBI
Mkuu wa zamani wa Polisi ya Upelelezi ya Marekani FBI amesema Rais Donald Trump wa nchi amekubuhu kwa urongo na tabia yake hiyo imechafua taswira na hadhi ya FBI.
James Comey aliyasema hayo jana mbele ya waandishi wa habari, baada ya kutoka kwenye kikao cha pili cha faragha cha Kamati ya Upelelezi ya Baraza la Seneti la Marekani na kuongeza kuwa, hakuna mtu anayepaswa kubebeshwa dhima ya kupoteza hadhi FBI ghairi ya Trump kutokana na tabia yake ya kusema urongo kila mara.
Amesema Trump anawadanganya wananchi kupitia jumbe zake anazoziandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na taratibu anahujumu utawala wa sheria wa nchi hiyo.
Mkuu huyo wa zamani wa FBI hivi karibuni alisema kuwa, mienendo ya Trump ni yenye kutia wasiwasi mkubwa na kwamba rais huyo hawezi kuiongoza Marekani kwa kutumia usambazaji wa jumbe kwenye mtandao huo wa kijamii.
Inafaa kuashiria kuwa, katika miezi ya hivi karibuni James Comey amekuwa katika vita vya maneno na Donald Trump.
Trump alimpiga kalamu nyekundu Comey mwaka jana kufuatia kashfa iliyoelekezwa kwa Trump kwamba alikuwa na uhusiano na Russia kuhusiana na uchaguzi wa rais uliopita nchini Marekani.