Matatizo ya wakimbizi wa Rohingya yaongezeka
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, kuanzishwa kambi yenye idadi kubwa ya wakimbizi Waislamu wa kabila la Rohingya wa Myanmar nchini Bangladesh ni hatari kubwa na umesisitiza kuwa, hatua hiyo inaweza kusababisha matatizo mengi ikiwa ni pamoja na kuenea magonjwa ya kuambukiza.
Serikali ya Bangladesh imetangaza kuwa, inataka kujenga kambi moja kwa ajili ya wakimbizi laki nane wa Rohingya waliokimbia mauaji yanayofanywa na Mabudha katika mkoa wa Rakhine. Awali serikali ya Dhaka ilikuwa imetangaza kuwa baadhi ya wakimbizi hao watapelekwa katika kisiwa cha mbali.
Maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar wamelazimika kukimbilia katika nchi jirani ikiwemo Bangladesh kutokana na mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Mabudha wenye misimamo mikali wakisaidiwa na jeshi la nchi hiyo hususan katika jimbo la Rakhine lililoko magharibi mwa nchi hiyo. Kwa sasa jinai na ukatili unaofanywa dhidi ya Waislamu hao vimechukua mwelekeo mpya na iwapo jamii ya kimataifa haitachukua hatua za haraka za kukomesha ukatili huo kuna uwezekano wa kushuhudiwa mauaji makubwa zaidi ya kimbari nchini Myanmar.
Hadi sasa maelfu ya Waislamu hao wameuawa na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa katika hujuma hiyo kubwa ya Mabudha wa Myanmar. Maelfu ya wakimbizi hao pia wanakabiliwa na matatizo makubwa hasa wale waliokimbilia misituni na wale wanaoelekea nchi jirani kwa njia ya bahari ambao wamekuwa wakizama kila siku kutokana na idadi kubwa kupanda boti zisizokuwa na viwango wakihofia kuuawa. Kambi za sasa za wakimbizi hao pia hazina suhula za msingi za kuishi mwanadamu na utapia mlo, ukosefu wa huduma za tiba na afya, maradhi na kadhalika vinahatarisha maisha ya maelfu ya wakimbizi hao. Watoto wa wakimbizi hao pia hawana shule wala huduma za kupata elimu.
Mtaalamu wa elimu jamii wa Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani, Profesa Saskia Sassen anasema: Kufukuzwa wakimbizi hao ni mbinu ya kutaka kutwaa ardhi na milki zao inayotumiwa na Mabudha. Mabudha hao pia wanachoma moto kila kitu kama mashamba na makazi yanayoachwa na wakimbizi Waislamu wa Rohingya ili kutatiza au kuzuia kabisa uwezekano wa kurekea katika maeneo walimokuwa wakiishi", mwisho wa kunukuu.
Serikali ya Bangladesh nayo imezidisha mashinikizo dhidi ya Wakimbizi hao wa Rohingya kwa kutoa tuhuma kama madai kwamba, wanasababisha matatizo ya kiusalama na kijamii. Serikali ya Dhaka inafuatilia malengo mawili katika suala hilo. Kwanza ni kuwabinya Waislamu hao na kwualazimisha kuodoka nchini humo au kuwatishia wale ambao hawajaingia nchini humo na kuwafanya wasielekee Bangladesh. Lengo la pili ni kujaribu kuzidisha matatizo ya wakimbizi hao kwa shabaha ya kupata misaada zaidi ya kimataifa.
Mtaalamu wa masuala ya wakimbizi wa Umoja wa Mataifa nchini Bangladesh Mark Pearce anasema: "Wakimbizi wengi wa Rohingya wamechoka na wanasumbulwia na njaa, hawana chakula wala maji. Hadi sasa hakujatolewa tathmini ya mahitaji ya chakula, makazi, dawa na kadhalika vinavyohitajiwa na wakimbizi kutokana na idadi yao kubwa na iwapo mahitaji yao hayatakidhiwa haraka hali ya wakimbizi hao Waislamu itakuwa mbaya zaidi".
Alaa kulli hal, japokuwa jamii ya kimataifa imelaani kwa maneno mauaji yanayofanywa dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya huko Myanmar na kueleza masikitiko yake kuhusu hali mbaya ya wakimbizi wa nchi hiyo, lakini hadi sasa hazijachukua hatua za maana za kuishinikiza serikali ya Myanmar na kuilazimisha kukomesha mauaji na kuwatambua rasmi Waislamu hao kama raia wenye haki kamili.