Korea Kaskazini yaionya Australia dhidi ya kushirikiana na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i35681-korea_kaskazini_yaionya_australia_dhidi_ya_kushirikiana_na_marekani
Korea Kaskazini imeionya Australia kuwa inajitafutia balaa kwa kushirikiana na Marekani na Korea Kusini kuishinikiza Pyongyang iachane na mipango yake ya nyuklia na makombora ya balestiki.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 15, 2017 07:57 UTC
  • Korea Kaskazini yaionya Australia dhidi ya kushirikiana na Marekani

Korea Kaskazini imeionya Australia kuwa inajitafutia balaa kwa kushirikiana na Marekani na Korea Kusini kuishinikiza Pyongyang iachane na mipango yake ya nyuklia na makombora ya balestiki.

Shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini (KCNA) limemnukuu Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa nchi hiyo akisema kuwa: "Hivi karibuni, tumeiona Australia ikichukua hatua hatari ya kujiingiza na kuunga mkono chokochoko za kijeshi na kisiasa za Marekani dhidi ya DPRK (Korea Kaskazini), iwapo itaendelea kufuata kibubusa mkondo huo wa US, basi ijiandae kwa balaa kubwa."

Kadhalika amemkosoa vikali Julie Bishop, Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia kwa kuunga mkono sera za Marekani na Korea Kusini, haswa kwa kauli yake kuwa kuna haja ya machaguo yote likiwemo la kijeshi kutumiwa dhidi ya Korea Kaskazini iwapo haitaachana na miradi yake ya nyuklia na kufanyia majaribio makombora ya balestiki.

Sehemu ndogo ya makombora ya balestiki ya Korea Kaskazini

Akijibu vitisho hivyo vya Korea Kaskazini, Waziri wa Masuala ya Maveterani wa Australia, Dan Tehan amesema Sydney haibabaishwi na kelele za Pyongyang na kwamba itaendelea kuwaunga mkono na kushirikiana na wapambe wake kwa hali na mali.

Marekani na Korea Kusini zinatazamiwa kuanza mazoezi ya kijeshi ya pamoja kuanzia kesho hadi Oktoba 26, katika Bahari ya Japan na Bahari ya Manjano, ikiwa ni muondelezo wa chokochoko dhidi ya Pyongyang.