Waislamu 7 wa Rohingya waghariki katika ajali nyingine ya boti
https://parstoday.ir/sw/news/world-i36072-waislamu_7_wa_rohingya_waghariki_katika_ajali_nyingine_ya_boti
Waislamu saba wa jamii ya Rohingya wamepoteza maisha katika ajali mbili tofauti za boti karibu na pwani ya Bangladesh wakikimbia mauaji na ukandamizaji unaofanywa dhidi yao na serikali ya Myanmar.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 31, 2017 13:25 UTC
  • Waislamu 7 wa Rohingya waghariki katika ajali nyingine ya boti

Waislamu saba wa jamii ya Rohingya wamepoteza maisha katika ajali mbili tofauti za boti karibu na pwani ya Bangladesh wakikimbia mauaji na ukandamizaji unaofanywa dhidi yao na serikali ya Myanmar.

Mkuu wa Polisi katika eneo la pwani la Bengal, Abul Khair amesema kwa akali watu wanne wamekufa maji baada ya boti yao kuzama karibu na pwani ya Bangaldesh leo Jumanne.

Imearifiwa kuwa, boti hiyo ambayo ilikuwa imebeba wakimbizi Waislamu 45 wa jamii ya Rohingya, imezama karibu na ufuo wa Inani, katika wilaya ya Cox's Bazar, mpakani mwa Bangladesh na Myanmar.

Wakati huo huo, watoto watatu wameaga dunia baada ya boti yao kuzama katika mji wa Teknaf jana Jumatatu. Mkuu wa polisi katika mji huo, Main Uddin amesema watoto hao walikuwa na umri kati ya miezi mitatu na kumi. 

Waislamu wa jamii ya Rohingya wakielekea Bangladesh

Hii si mara ya kwanza kwa wakimbizi Waislamu wa Rohingya kufariki dunia katika ajali za boti, wakikimbilia usalama wao katika nchi jirani ya Bangaldesh. Zaidi ya wakimbizi 200 wa jamii ya Rohingya wamekufa maji katika ajali hizo, karibu na pwani ya Bengal, katika mpaka wa nchi mbili hizo.

Maelfu ya Waislamu wa Rohingya wameuawa na malaki ya wengine wamelazimishwa kuwa wakimbizi katika nchi jirani ya Bangladesh tangu tarehe 25 mwezi Agosti mwaka huu, kutokana na mauaji yanayofanywa na Mabudha wenye misimamo mikali wakishirikiana na jeshi la serikali ya Myanmar katika mkoa wa Rakhine.