Trump: Nilikuwa sijui kwamba duniani kuna nchi nyingi kiasi chote hiki
Rais wa Marekani, Donald Trump amedhihirisha kwa uwazi ujinga na upofu wake kuhusiana na elimu ya jiografia na siasa za kimataifa aliposema bila matani kwamba alikuwa hajui kuwa duniani kuna nchi nyingi kiasi chote hiki mpaka alipochaguliwa kuwa rais wa Marekani.
Trump alibwatuka hivyo siku ya Jumatatu katika hotuba yake aliyoitoa mbele ya viongozi na watu muhimu nchini Japan katika hatua ya kwanza ya ziara yake barani Asia na kukiri hadharani kwamba alikuwa hajui duniani kuna nchi ngapi mpaka alipoanza kupokea simu za pongezi kutoka kwa viongozi wa nchi mbalimbali baada ya kuchaguliwa kuwa rais wa Marekani, hapo ndipo alipogundua kwamba, kumbe duniani kuna nchi nyingi sana.
Mfanyabiashara huyo asiye na welewa wowote wa siasa wala mambo yanayovyokwenda duniani alitangazwa mshindi wa urais wa Marekani katika mazingira ya kutatanisha na hadi leo hii amekuwa akitoa matamshi yaliyojaa utata na kuchukua hatua zinazoonesha jinsi alivyo mwanagenzi sana katika masuala ya siasa na uhusiano wa kimataifa.
Trump aliendelea kujianika hadharani kwa kusema: "Nilikuwa sijui kwamba ilikuwa huwezi kuonana na viongozi wa dunia hadi pale unapoingia Ikulu.
Upayukaji huo wa Trump umeenea kwenye mitandao ya kijamii na kuzusha hasira na istihzai kubwa kutoka kwa watumiaji wa mitandao hiyo.
Ziara ya Trump nchini Japan ilikuwa sehemu ya ziara yake ya siku 12 ya kuzitembelea nchi kadhaa za Asia katika juhudi za kuzikinaisha nchi hizo kuiwekea mashinikizo Korea Kaskazini kadiri inavyowezekana kutokana na miradi yake ya nyuklia na makombora.
Ziara hiyo ya Trump ni ya kutembelea nchi tano za Asia ambazo ni Japan, Korea Kusini, China, Vietnam na Ufilipino.