Rais wa Bangladesh aikosoa Myanmar
Rais wa Bangladesh amekosoa vikali vitendo vya utumiaji mabavu vya jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.
Muhammad Abdul Hamid amesema hayo mjini Dhaka katika mazungumzo yake na Papa Francis Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani na kueleza kuwa, maelfu ya wanaume, wanawake na watoto Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar wameuawa kinyama na jeshi pamoja na Mabudha wa nchi hiyo wenye misimamo mikali.
Kama alivyosema Rais wa Bangladesh ni kuwa, katika jinai za jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu Warohingya kuna wanawake waliobakwa na kunajisiwa na wanajeshi pamoja na Mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada huku nyumba zao zikichomwa moto katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa nchi hiyo.
Rais Muhammad Abdul Hamid wa Banglesh ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia ili Waislamu wa jamii ya Rohingya waweze kurejea katika makazi yao. Safari ya Papa Francis Kiongozi wa Kanisa Katoliki huko Mynamar na Bangladesh imefanyika katika hali ambayo, hivi karibuni Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch lilitoa ripoti yenye kuonyesha kwamba, kuna ushahidi unaofichua bayana kwamba, kumefanyika jinai na mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya. Katika wiki za hivi karibuni, viongozi wa kisiasa na kidini wa Ulaya wamejitoa kimasomaso na kuonyesha sura ya ubinadamu ambapo wamefanya safari huko Myanmar na Bangladesh na kutembelea kambi za wakimbizi za Waislamu wa jamii ya Rohingya.
Hata hivyo katika matamashi yao si tu kwamba, hawakuionyeshea kidole cha tuhuma serikali ya Myanmar kutokana na kutenda jinai za kivita na mauaji ya kimbari, bali walinyamazia kimya hilo na wakati huo huo hatua yao ya kuitaka serikali ya Bangladesh ishughulikie hali ya wakimbizi wa jamii ya Rohingya, kivitendo ililishajiisha jeshi na serikali ya Myanmar iendelee na jinai zake dhidi ya Waislamu hao madhulumu.
Hii ni katika hali ambayo, Waislamu wa jamii ya Rohingya wanachohitajia ni kuchukuliwa hatua za kivitendo na jamii ya kimataifa kwa ajili ya kuhitimisha mauaji ya umwagaji damu ya jeshi na serikali dhidi yao.
Yanghee Lee ripota maalumu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa anasema: Madai ya serikali ya Myanmar kwamba, Waislamu Warohingya walichoma nyumba zao wao wenyewe, hayana itibari na si kweli; na bila shaka muamala wa polisi wa Myanmar na vitendo vyao vya kuwapiga, kuwanyanyasa na kushambulia vijiji vya Waislamu ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu ambao unapaswa kukomeshwa haraka iwezekanavyo.
Kwa mtazamo wa duru za Magharibi inaonekana kuwa, serikali ya Myanmar imefanikiwa kuwafurusha Waislamu wa jamii ya Rohingya kutoka katika nyumba zao na hivi sasa hali katika jimbo la Rakhine ambalo linahesabiwa kuwa ni ardhi ya mababu za Waislamu hao, iko tayari kwa ajili ya uwekezaji. Hii ina maana kuwa, serikali ya Myanmar inatekeleza mipango yake ya kiuchumi katika maeneo ambayo ni miliki ya Waislamu wa Rohingya. Hata hivyo hatua ya kuwaua na kuwafanya wakimbizi Waislamu hao ina lengo la kukiangamiza kizazi cha Waislamu hao katika jimbo hilo na nchi za Magharibi zinakaribisha kwa mikono miwili jambo hilo.
Phil Robertson mtaalamu wa masuala ya kimataifa anaamini kuwa: Waislamu wa jamii ya Rohingya wamekuwa wakiandamwa na mashambulio makali. Serikali ya Myanmar inapaswa kukomesha mara moja mashambulio hayo.
Alaa kulli haal, Rais wa Bangladesh anakosoa kuendelea mauaji dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya yanayofanywa na serikali na jeshi la Myanmar katika hali ambayo, licha ya malalamiko ya jamii ya kimataifa, mwenendo huo ungali unaendelea, huku serikali ya Myanmar ikiwa mbioni kukamilisha mwenendo wa mauaji ya kimbari na kuangamiza kizazi katika jimbo la Rakhine.
Hapana shaka kuwa, safari za viongozi mbalimbali zinazofanyika huko Myanmar ambazo bila shaka ni kwa ajili ya kupiga picha za ukumbusho tu, katu haziwezi kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayowakabili Waislamu hao. Kudiriki ukweli huo ndiko kulikoibua malalamiko ya viongozi wa Bangladesh na kuitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua za maana ili kuandaa mazingira ya kurejea wakimbizi wa Rohingya katika makazi yao.