Uhispania: Kuna udharura wa kila nchi kupambana na Daesh
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania, José Manuel García-Margallo amezitaka nchi zote duniani kupambana vilivyo na kundi la kigaidi la Daesh kwa ajili ya kukomesha tatizo hilo.
Manuel García-Margallo ameyasema hayo katika mahojiano na gazeti la The Larson ambapo ameashiria mashambulizi ya hivi karibuni ya wafuasi wa kundi hilo mjini Brussels, Ubelgiji na kusema kuwa, genge hilo ni tofauti na makundi mengine ya kigaidi hasa kutokana na kuwa na muundo mithili ya serikali ya nchi. Kwa mujibu wa waziri huyo wa mambo ya nje wa Uhispania, kundi hilo la kigaidi lina mtandao wa ajabu wa kuvutia vijana kujiunga nalo kama ambavyo pia lina bajeti kubwa ya kifedha. Ameongeza kuwa, kundi hilo ambalo hii leo ulimwengu umekumbwa na hujuma na mashambulizi yake, limekuwa likitumia vyombo vyake vya kipropaganda kuwavutia watu kujiunga nalo. Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo wa Uhispania, mbali na ushirikiano wa idara za kijasusi, kila nchi inatakiwa kuchukua hatua za kukabiliana na genge hilo la kigaidi na kuwafuatilia wanachama wake popote pale duniani. Matamshi ya waziri wa mambo ya nje wa Uhispania yanatolewa katika hali ambayo ni nchi za Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu na za eneo la Mashariki ya Kati ndio waungaji mkono wakuu wa kifedha, kisilaha na kilojestiki wa makundi ya kigaidi na kitakfiri yanayofanya jinai nchini Syria, Iraq na Lebanon. Katika shambulio la Jumanne iliyopita, watu 34 waliuawa na zaidi ya wengine 200 kujeruhiwa huko Brussels, mji mkuu wa Ubelgiji.