Marekani yakiri kuwa haiwezi kuingia kwenye vita vya kijeshi na Iran
Waziri wa Ulinzi wa Marekani amekiri kuwa Washington haina mpango wowote wa kuanzisha vita vya kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na tuhuma kuwa Tehran inaizatiti kwa silaha harakati ya Ansarullah ya Yemen.
Akijibu swali la waadishi wa habari katika makao makuu ya Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo (Pentagon) jana Jumamosi, waliomtaka aeleze iwapo Marekani inatathmini kuichukulia Iran hatua ya kijeshi eti kwa kupatikana 'ushahidi' wa kuizatiti kwa makombora ya balestiki Ansarullah ya Yemen, James Mattis alisema: "Hapana! Hatutaishambulia kijeshi. Tutatumia jitihada za kidiplomasia kuionyesha dunia kile ambacho Iran inaazimia kufanya na ndiposa tumemtuma Balozi Halley na sio mmoja wa majenerali wetu,"
Alkhamisi iliyopita, huku akiwa amesimama kando ya mabaki ya vyuma, Nikki Haley, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa alianzisha propaganda mpya dhidi ya Iran kwa kudai kwamba vyuma hivyo ni mabaki ya makombora ya Iran, yaliyotumiwa na harakati ya Ansarullah ya Yemen kuishambulia Saudia.
Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itawasilisha malalamiko yake kwa Umoja wa Mataifa dhidi ya madai hayo yaliyotolewa na Marekani.
Kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani, tangu mwezi Machi mwaka 2015 Saudi Arabia ilianzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa ardhini, baharini na angani, ambapo hadi sasa makumi ya maelfu ya watu wameuawa na kujeruhiwa na mamilioni ya wengine kubaki bila makazi.