Kaburi la umati la Waislamu lagunduliwa nchini Myanmar
Kaburi la umati limepatikana nchini Myanmar katika eneo ambalo Waislamu wa jamii ya Rohingywa wamekuwa wakilengwa na kuuawa kiholela katika mashambulizi yanayoungwa mkono na serikali katika kipindi cha mwaka mmoja sasa.
Jeshi la Myanmar na Mabudha wenye misimamo mikali wamekuwa wakiteketeza moto vijiji vya Waislamu katika jimbo la Magharibi la Rakhine tokea Novemba mwaka jana. Waislamu wamekuwa wakiuawa kiholela, wanawake kunajisiwa na maelfu kujeruhiwa katika kile Umoja wa Mataifa umekitaja kuwa ni 'mauaji ya kimbari."
Wimbi hilo la mauaji lilishika kasi kuanzia Agosti 25 ambapo taarifa zinasema katika kipindi cha mwezi mmoja tokea wakati huo, Waislamu zaidi ya 6,500 wameuawa na wengine karibu laki saba kukimbilia katika nchi jirani ya Bangladesh.
Duru zinadokeza kuwa kaburi la umati limepatikana katika kijiji cha Inn Dinn katika mji wa Maungdaw, sehemu ambayo imeshuhudia jinai mbaya zaidi zikitekelezwa dhidi ya Waislamu.
Baada ya kuenea habari za kaburi hilo la umati, mkuu wa Jeshi la Myanmar amedai kuwa, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya afisa yeyote wa usalama aliyehusika.
Siku ya Jumanne, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilichapisha ripoti ya mauaji ya makusudi ambayo yamekuwa yakitekelezwa na jeshi la Myanmar katika jimbo la Rakhine.