Mbunge wa Democratic nchini Marekani asema Trump ni tapeli
Mbunge wa chama cha Democrats nchini Marekani amesema Rais Donald Trump wa nchi hiyo ni mtu tapeli na laghai.
Gregory Meeks amesema kitendo cha rais huyo wa Marekani kuunga mkono muswada uliopasishwa hivi karibuni kuhusu masuala ya utozaji wa ushuru, kinaashiria namna mwanasiasa huyo wa Republican alivyo tapeli.
Amesema sheria hiyo iwapo itatekelezwa, inalenga kuendelea kuwatajirisha mabwenyenye wa chama cha Repulican akiwemo Trump mwenyewe na kuwaumiza Wamarekani wa vipato vya wastani.
Katika mahojiano na kanali ya televisheni ya CNN hapo jana, mwakilishi huyo wa New York amesema, na hapa tunanukuu: "Tangu hapo awali nimekuwa nikisisitiza kuwa huyu rais (Trump) ni tapeli. Anakupa kitu kinachoonekana kina maslahi na wewe, lakini mwishowe kinakuja kukuathiri. Lazima uwe makini na mwangalifu sana kwa kuwa Trump ni laghai wa kuuma na kupuliza."
Amefafanua kuwa, sheria hiyo ikianza kutekelezwa, asilimia 8 ya kodi itakayopunguzwa, itanufaisha asilimia 1 ya matajiri mabilionea wa nchi hiyo.
Tafiti nyingi za maoni za hivi karibuni zinaonyesha kuwa, Wamarekani wengi hawauungi mkono Muswada wa Kodi wa GOP ambao Trump amekuwa akiupigia debe katika majukwaa mbali mbali.