Basi lateketea na kuua abiria 52 nchini Kazakhstan
Watu wasiopungua 52 wamepoteza maisha baada ya basi la abiria kuteketea moto kaskazini mwa Kazakhstan.
Maafisa wa serikali ya nchi hiyo wamesema ajali hiyo imetokea alfajiri ya leo Alkhamisi katika kijiji cha Kalybai, eneo la Aktobe lililoko kaskazini mwa nchi.
Inaarifiwa kuwa, basi hilo lilikuwa linatoka katika mji wa Shymkent, kusini mwa nchi likielekea upande wa kaskazini, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Uzbekstan.
Habari zaidi zinasema, wahanga wote wa mkasa huo walikuwa raia wa nchi jirani ya Uzbekistan. Watu wawili miongoni mwa walionusurika ni madereva raia wa Kazakhstan, ambao walikuwa wanaliendesha gari hilo kwa kupokezana.
Idara ya Kushughuikia Majanga nchini humo imesema abiria watano kati ya 57 waliokuwemo kwenye basi hilo ndio waliofanikiwa kukwepa ndimi za moto huo mkali ulioteketeza basi hilo.
Kiini cha moto huo hakijajulikana lakini timu ya wachunguzi inasema yumkini ulisababishwa na hitilafu za kiufundi.