Feb 19, 2018 15:39 UTC
  • Waziri Mkuu wa Uingereza atembelea msikiti akiwa amevaa mtandio kichwani

Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May ametembelea msikiti mmoja mjini London akiwa amevaa mtandio kichwani ikiwa ni sehemu ya kushiriki katika kampeni maalumu ya Waislamu wa Uingereza inayoendeshwa chini ya kaulimbiu ya "Tembelea Msikiti Wangu."

Zaidi ya misikiti 200 katika kona mbalimbali za Uingereza imeanzisha kampeni hiyo kwa ajili ya kuwaelimisha wafuasi wa dini nyinginezo sura halisi ya Uislamu na kupambana na magenge yanayoeneza chuki dhidi ya Waislamu.

Taasisi ya Kiislamu ya Uingereza ambayo iko chini ya ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, nayo inashiriki kwenye kampeni hiyo. ambayo inafanyika tarehe 18 Februari kila mwaka.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May alipotembelea Msikiti wa al Madina mjini London 2015

 

Waziri Mkuu wa Uingereza ametembelea pia Msikiti wa Bustani ya Finsbury sehemu ambayo basi moja dogo liliwahi kuvamia kundi la Waislamu waliokuwa wanatoka msikiti kusali mwezi wa Ramadhani, kitendo ambacho kilithibitika baadaye kuwa ni cha kigaidi kilichofanywa na mtu mwenye chuki za kidini.

Mwenyekiti wa msikiti huo Mohammed Kozbar, pamoja na viongozi wa dini nyinginezo wamekaa kimya kwa sekunde kadhaa kama njia ya kuwakumbuka Waislamu walioshambuliwa katika uvamizi wa basi hilo dogo katika mwezi huo mtukufu wa Ramadhani.

Baada ya kumalizika sekunde hizo za kuwakumbuka wahanga wa shambulio hilo, Mohammed Kozbar amesoma risala fupi na kusisitiza kuwa, kuwashambulia watu wa imani fulani ni sawa na kuwashambulia watu wa imani zote.

Tags