Mogherini: Mgogoro wa Syria hauna ufumbuzi wa kijeshi
Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa mgogoro wa Syria unaweza tu kupatiwa ufumbuzi kwa njia za kisiasa.
Federica Mogherini amesema leo kuwa Umoja wa Ulaya kwa mara nyingine tena unasisitiza kuwa kushadidisha hali ya machafuko nchini Syria kunaweza kusababisha makabiliano makubwa zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati yatakayokuwa na taathira kubwa kwa kanda hiyo na ulimwengu mzima kwa ujumla.
Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesisitiza katika taarifa yake kuwa umoja huo unaamini kuwa, njia yoyote ya kuupatia ufumbuzi wa kudumu mgogoro wa Syria inahitaji kipindi halisi cha mpito cha kisiasa kwa mujibu wa azimio nambari 2254 la mwaka 2012 la mjini Geneva Uswisi, ambalo limekuwa likijadiliwa na pande zote za Syria katika fremu ya mchakato wa Geneva na chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.
Wakati huo huo msemaji wa Federica Mogherini amesema kuwa kadhia ya Syria itachunguzwa Jumatatu wiki hii katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Ulaya huko Luxembourg.