Ripoti ya Antonio Guterres: Jeshi la Myanmar liliwabaka Waislamu Warohingya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i43132-ripoti_ya_antonio_guterres_jeshi_la_myanmar_liliwabaka_waislamu_warohingya
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, jeshi la Myanmar lilitumia suala la ubakaji kama wenzo wa kuwafanya Waislamu wa jamii ya Rohingya wayakimbie makazi yao.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 15, 2018 07:55 UTC
  • Ripoti ya Antonio Guterres: Jeshi la Myanmar liliwabaka Waislamu Warohingya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, jeshi la Myanmar lilitumia suala la ubakaji kama wenzo wa kuwafanya Waislamu wa jamii ya Rohingya wayakimbie makazi yao.

Antonio Guterres amesema kuwa, vitisho na kuwabaka wanawake Waislamu wa Rohingya ilikuwa sehemu ya mikakati ya jeshi la Myanmar ambayo ilipelekea kuzusha hofu miongoni mwa jamii hiyo na kuwafanya wayakimbie makazi yao.

Ripoti hiyo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa imetolewa siku moja tu baada ya kurejea nchini Myanmar familia ya kwanza ya wakimbizi hao Waislamu waliokimbilia katika nchi jirani ya Bangladesh.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, huko nyuma pia ripoti mbalimbali za Umoja wa Mataifa zimekuwa zikisisitiza kwamba,  jeshi la Myanmar limekuwa likitumia mbinu mbalimbali za ukatili, mauaji na kubaka wanawake Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo kama njia ya kuwalazimisha wayakimbie makazi yao.

Waislamu wa Myanmar baada ya kuyakimbia makazi yao

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) pia limewahi kusema kuwa, jeshi la Myanmar linawaua kiholela na kuwanajisi Waislamu wa jamii ya Rohingya magharibi mwa nchi hiyo.

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo tangu tarehe 25 Agosti mwaka huu hadi sasa. Mauaji hayo ya umati dhidi ya Waislamu nchini Myanmar yamepelekea zaidi ya nusu milioni kati yao kukimbilia hifadhi katika nchi jirani ya Bangladesh.