Mvua, radi na vimbunga vyaua watu 143 nchini India
https://parstoday.ir/sw/news/world-i44022-mvua_radi_na_vimbunga_vyaua_watu_143_nchini_india
Wimbi la vimbunga vilivyoikumba India wiki hii limesababisha vifo vya watu wasiopungua 143, huku maafisa wa serikali wakitahadharisha kuwa yumkini idadi hiyo ikaongezeka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 04, 2018 02:52 UTC
  • Mvua, radi na vimbunga vyaua watu 143 nchini India

Wimbi la vimbunga vilivyoikumba India wiki hii limesababisha vifo vya watu wasiopungua 143, huku maafisa wa serikali wakitahadharisha kuwa yumkini idadi hiyo ikaongezeka.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa imeonya leo Ijumaa kuwa, vimbunga hivyo vinatazamiwa kushika kasi kesho Jumamosi hususan katika maeneo ya kusini mwa nchi.

Watu 121 wamepoteza maisha kufikia sasa katika maeneo ya Uttar Pradesh, Rajasthan, Uttarakhand na Punjab, huku wengine 21 wakiaga dunia baada ya radi kupiga eneo la kusini mwa nchi mara 40,000.

Majanga hayo ya kimaumbile pia yameathiri maeneo ya Saharanpur, Bareilly, Bijnore na Agra katika jimbo la Uttar Pradesh.

Sehemu ya athari za vimbunga nchini India

Munna Lal Jha, mkazi wa eneo la Agra ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, "Tulichukua tahadhari mapema kuhusu janga hili lililokuwa likitukodolea macho, lakini hakuna matu anayeweza kushindana na ghadhabu za kimaumbile."

Mkuu wa Idara ya Kupambana na Majanga nchini humo, R V Chandravadan, amesema ingawaje mvua, radi na vimbunga huua maelfu ya watu kila mwaka nchini Indian, lakini majanga hayo yameoenekana kushika kasi mwaka huu.