Katibu Mkuu wa UN: JCPOA ni ushindi muhimu wa kidiplomasia
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya dhidi ya kuvunjwa makubaliano ya nyuklia ya Iran huku akisisitiza kuwa mapatano hayo ni ushindi muhimu wa kidiplomasia ambayo yanapaswa kulindwa.
Katika mahojiano na idhaa ya BBC Radio 4 jana Alkhamisi, Antonio Guterres alisema, "Nadhani JCPOA ulikuwa ushindi wa kistratajia na wa kidiplomasia na sidhani tunapaswa kuyafuta makubaliano hayo katika hali ambayo hatuna chaguo mbadala."
Katibu Mkuu wa UN amebainisha kuwa, kutokana na hali nyeti ya eneo la Mashariki ya Kati na ushawishi wa Iran katika eneo hilo, kuna haja kuyapa kipaumbele mazungumzo ya maana.
Rais Donald Trump wa Marekani ambaye amekuwa akiyaponda mapatano hayo anatazamiwa Mei 12 kutangaza iwapo nchi hiyo itajiondoa kwenye mapatano hayo au la.
Hata hivyo pande zingine zote za makubaliano hayo zimekuwa zikisisitiza mara kwa mara kuhusu umuhimu wa pande zote husika kuendelea kufungamana na mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kwa kifupi kama JCPOA.
Ripoti zote za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) zimeonyesha kuwa Iran imendelea kufungamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, yaliyoanza kutekelezwa Januari mwaka 2016.