Waislamu India wazidi kuwekewa vizuizi vya kutekeleza nguzo ya Sala
https://parstoday.ir/sw/news/world-i44216-waislamu_india_wazidi_kuwekewa_vizuizi_vya_kutekeleza_nguzo_ya_sala
Katika mwendelezo wa mpango wa kuzidi kuwabana Waislamu nchini India na kuwawekea mipaka ya uhuru wa kuabudu, serikali ya jimbo la Haryana imetangaza kuwa ni marufuku Waislamu kusali katika maeneo mengine ghairi ya misikitini.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
May 08, 2018 12:26 UTC
  • Waislamu India wazidi kuwekewa vizuizi vya kutekeleza nguzo ya Sala

Katika mwendelezo wa mpango wa kuzidi kuwabana Waislamu nchini India na kuwawekea mipaka ya uhuru wa kuabudu, serikali ya jimbo la Haryana imetangaza kuwa ni marufuku Waislamu kusali katika maeneo mengine ghairi ya misikitini.

Manohar Lal Khattar, Waziri Kiongozi wa jimbo la Haryana lililoko kaskazini mwa India ametangaza kuwa ibada ya Sala ikiwemo Sala ya Ijumaa isaliwe ndani ya misikiti tu na ni marufuku kusaliwa katika maeneo ya umma.

Waziri Kiongozi wa jimbo la Haryana ameongeza kuwa: Utekelezaji ibada ya Sala katika maeneo ya umma umekuwa ukiongezeka; na kama Waislamu hawana sehemu za kutosha za kusalia Sala zao za jamaa itawapasa wafanye ibada zao hizo ndani ya nyumba zao kila mtu peke yake.

Matamshi hayo ya kiongozi huyo wa jimbo la Haryana yametolewa siku chache tu baada ya wafuasi wa kundi moja lenye misimamo ya chuki dhidi ya Waislamu katika jimbo hilo kuwashambulia Waislamu waliokuwa wakisali Sala ya Ijumaa katika eneo la Gurugram.

Waziri Kiongozi wa jimbo la Haryana, Manohar Lal Khattar

Imeripotiwa kuwa kuna maeneo ya wazi yapatayo 115 yanayotumiwa na Waislamu wa jimbo la Haryana kwa ajili ya Sala za jamaa. Waislamu hao wanalalamika kuwa jimbo hilo lina uhaba wa misikiti kwa ajili ya waumini wapatao laki sita wanaoishi katika jimbo hilo.

Tangu chama cha Bharatiya Janata kiingie madarakani nchini India mashambulio ya makundi ya Wahindu wenye misimamo ya kufurutu mpaka na chuki dhidi ya Uislamu yameongezeka, ambapo hadi sasa makumi ya Waislamu wameuawa katika hujuma na mashambulio hayo.../